Kumekucha! Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na hatua iliyofikiwa kwenye Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHP).
Serikali imesema itaanza kuruhusu maji kujaa kwenye bwawa hilo kuanzia Desemba 15 mwaka huu yaani siku tisa zijazo, huku matarajio ya kujaa kwa kiwango kitakachowezesha kuzalisha umeme yakiwa ni Aprili mwakani.
Ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 77.15 na itakapofika tarehe ya kuanza kuruhusu maji, utafikia zaidi ya asilimia 80, huku kukamilika kwa mradi na kazi ya kufua umeme kukitarajiwa kuwa Juni 14, 2024. Mradi huo utakaogharimu zaidi ya Sh. trilioni 6.5 ukiwa na uwezo wa kufua megawati 2,115 za umeme.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi hadi sasa kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari waliotembelea eneo la mradi kuona maendeleo yake, Mhaifrolojia David Munkyala alisema kazi hiyo inasimamiwa kwa karibu na umakini na makandarasi wazawa kwa kushirikiana na makandarasi Arab Contractor na Elsewedy Electric.
Alisema wataanza kujaza maji wiki ya pili ya mwezi huu kwa kuwa utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), umeonesha kutakuwa na mvua nyingi ambazo zitaendelea hadi Aprili mwakani, na kama lisipojazwa sasa itakuwa vigumu kwa mwaka unaofuata.
“Kwa kiasi kikubwa kazi inakwenda kwa kasi kubwa, tunajitahidi tuwezavyo ifanyike kwa haraka na kwa ubora mkubwa, tumeshakamilisha ukuta maalum wa kuzuia na kuwezesha bwawa kupata maji, sasa tunaziba pale tulikochepusha mto tunaurudisha kwenye njia yake halisi maji yaanze kujaa,” alisema.
Kwa mujibu wa Munkyala, kuna kiwango cha maji kinatakiwa kujaa ndipo uzalishaji uanze ni urefu wa mita 163 na kiwango cha juu ni mita 184 kutoka usawa wa bahari huku ujazo wa bwawa ni mita bilioni 32.7, na kwamba kuna utaratibu wa kisasa wa kuzuia maji bila kuathiri kuta za mradi.
Alisema wakati wa kujaza maji hakutazuia shughuli nyingine za utumiaji maji kusimama kwa kuwa wananchi wanaoendesha shughuli zao na viumbe vinavyotegemea mto Rufiji baada ya eneo la mradi watendelea kupata maji kama kawaida.
Mkandarasi huyo alisema teknolojia ya ujenzi wa bwawa hilo ni ya kisasa na litaishi kwa zaidi ya miaka 100, uwezekano wa uchafu kujaa ndani na kuathiri uzalishaji ni mdogo kwa kuwa walifanya utafiti wa maji yanayoingia Mto Rufiji kutoka kwenye mikoa 10 na kubaini ni kidogo sana.
Aidha, alisema Watanzania wamepewa kipaumbele kwenye mradi kwa kutoa huduma, ulinzi, chakula, malighafi kama saruji tani 850,000, rebars tani 70,000 na pozzolana tani 250,000.
Naye Kaimu Mkurugenzi Huduma kwa Wateja wa Shirikal la Umeme Tanzania (TANESCO), Martin Mwambene, alisema maji ya kujaza bwawa hilo yanategemewa kutoka mikoa 10 nchini ambayo ni Tabora, Pwani, Singida, Morogoro, Mbeya, Lindi, Ruvuma, Iringa, Njombe na Dodoma.
“Tunaiomba jamii itumie maji kwa utaratibu endelevu kwamba kuna watumiaji wengine likiwamo bwawa hili lililojengwa kwa fedha zetu Watanzania na wananchi wanaotegemea Mto Rufiji kuendesha maisha yao, tupande miti na kutunza mazingira kwa faida ya wote,” alisema.
Alisema kujaa kwa bwawa hilo kunategemea mvua na chemchem nyingine na kwamba kukiwa na matumizi endelevu umeme utapatikana na kuchagiza shughuli za uchumi kwa wananchi wengi kuachana na shughuli hatari kwa mazingira na kutumia nishati hiyo kujinufaidha kiuchumi.
“TANESCO tunatoa elimu kila siku kwamba megawati moja, mti mmoja, maana yake tuwajibike kupanda miti na kulinda iliyopo. Tunashirikiana na wizara nyingine kuelimisha umma kuwa na matumizi endelevu,” alisema.
Mkataba wa ujenzi wa JNHP ulisainiwa Desemba 15, mwaka 2018, ikiwa ni kazi ya miezi 42 kati yake sita ni ya kujiandaa na 36 ya ujenzi, kazi ilianza rasmi Juni 15, mwaka 2019 na ilitakiwa kukamilika Juni 14, mwakani, lakini kutokana na kuchelewa kwa baadhi ya vifaa kutoka nje kwa sababu mbalimbali ikiwamo COVID uliongezwa mwaka mmoja.
Mradi huo umeajiri jumla ya watu 12,298 huku 11,190 sawa na asilimia 90.99 ni Watanzania na 1,108 sawa na asilimia 11.01 ni raia wa kigeni.