Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kubenea mbaroni kwenye basi, kujibu mashitaka 2

Kubentgea Kubenea mbaroni kwenye basi, kujibu mashitaka 2

Tue, 8 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Saed Kubenea, amekamatwa na kushitakiwa kwa makosa mawili likiwemo la kuingiza nchini fedha za kigeni kinyume na sheria.

Katika kosa la kwanza, Kubenea anadaiwa kukiuka Kanuni za Utoaji Tamko la Fedha Mpakani za mwaka 2016.

Kosa lingine ni kuingia nchini kinyume na Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54 Marejeo ya mwaka 2016.

Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, Biswalo Mganga alibainisha hayo jana kupitia taarifa kwa vyombo vya habari.

Biswalo alisema Jeshi la Polisi lilimkamata Kubenea Septemba 5 mwaka huu akiwa na Dola za Marekani 8,000, Sh 491,700 za Kenya na Sh 71,000 za Tanzania.

Alisema Kubenea alikamatwa siku hiyo akiwa kwenye gari la abiria lenye namba za usajili T 645 DKR, akitoka kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Namanga akienda mjini Arusha.

Biswalo alisema baada ya upekuzi, mtuhumiwa alikutwa na kiasi hicho cha fedha na tiketi ya basi la Super Coach lenye namba ya usajili KCP 4230 ya tarehe 05/09/2020 kutoka Nairobi, Kenya kwenda Namanga na ‘Memorandum of Understanding’ kati ya Hali-Halisi (Tanzania) na Buni Media Limited (Kenya).

Kitu kingine alichokutwanacho ni risiti ya malipo ya hoteli iitwayo After 40 Hotels Limited iliyopo Nairobi nchini Kenya.

Risti hiyo ina jina la Kubenea, Saed Ahmed kama mgeni kuanzia tarehe 3/9/2020 hadi 5/9/2020 na pasi yake ya kusafiria.

“Mara baada ya kukamatwa, mtuhumiwa alieleza kuwa alifika mkoani Arusha tarehe 2/9/2020 akitokea Dar es Salaam na kufikia katika hoteli iliyopo Arusha mjini. Alieleza zaidi kuwa tarehe 3/9/2020 alienda kulala kwa kaka yake tarehe 3/9/2020 na tarehe 4/9/2020 alienda Namanga na kupokea fedha taslimu tajwa hapo juu kutoka kwa raia wa Kenya,”alieleza Biswalo kwenye taarifa hiyo na kuongeza;

“Hata hivyo, mara baada ya kupitia ushahidi uliokusanywa nimebaini kuwa mtuhumiwa SAED AHMED KUBENEA hakufikia katika hoteli aliyoitaja Arusha mjini, wala kulala kwa kaka yake kama alivyoeleza. Mtuhumiwa tajwa alivuka mpaka usio rasmi na kuelekea Nairobi nchini Kenya na kisha kurejea nchini Tanzania bila kutumia mpaka rasmi mnamo tarehe 5/9/2020”ilieleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa Mganga, mtuhumiwa aliingiza nchini kiasi hicho cha fedha za kigeni bila kutoa tamko rasmi la kisheria kinyume na masharti ya kanuni za makubaliano ya kudhibiti utakatishaji fedha haramu za mwaka 2016 zikisomwa pamoja na Kifungu cha 28B (1) (a) cha Sheria ya Kuzuia Utakatishaji wa Fedha Haramu Na. 12 ya Mwaka 2006.

Alisema baada ya kujiridhisha na uwepo wa ushahidi wa kutosha dhidi ya mtuhumiwa sambamba na misingi ya kikatiba inayomwongoza kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 59B(4)(a) hadi (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, jana aliidhinisha mashitaka mawili dhidi ya Kubenea.

Chanzo: habarileo.co.tz