Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kubenea mbaroni kwa tuhuma za utakatishaji zaidi ya milioni 28

90fe85678ad582c256f8a8a1c497b1f8 Kubenea mbaroni kwa tuhuma za utakatishaji zaidi ya milioni 28

Mon, 7 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA Ubunge jimbo la Kinondoni kupitia ACT Wazalendo, Saed Kubenea anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuingiza nchini fedha za kigeni zenye thamani zaidi ya Sh milioni 28 za kitanzania bila kutoa tamko kinyume na Kanuni za Utoaji Tamko la Fedha Mpakani za mwaka 2016.

Pia anatuhumiwa kuingia nchini Tanzania kutoka Kenya mnamo Septemba 5, 2020 kinyume na Sheria ya Uhamiaji, Sura ya 54 Marejeo ya mwaka 2016.

Pia anatuhumiwa kuingiza nchini fedha za kigeni zenye thamani zaidi ya Sh milioni 28 za kitanzania bila kutoa tamko kinyume na Kanuni za Utoaji Tamko la Fedha Mpakani za mwaka 2016.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka iliyotolewa leo Septemba 7, 2020, Mkurugenzi wa Mshataka, Biswalo Mganga ameidhinisha mashtaka hayo dhidi ya Kubenea mara baada ya kujiridhisha na uwepo wa ushahidi wa kutosha dhidi yake .

Amesema kuwa alibaini kuwa Kubenea alivuka mpaka usio rasmi na kuelekea Nairobi nchini Kenya na kisha kurejea nchini Tanzania bila kutumia mpaka rasmi mnamo Septemba 05 mwaka huu.

Sambamba na hilo pia aligundua kuwa Kubenea aliingiza nchini Fedha za Kigeni (foreign currency) bila kutoa tamko rasmi la kisheria kinyume na masharti ya Kanuni za the Anti-Money Laundering (Cross - Border Declaration of Currency and Bearer Negotiable Instruments) Regulations, 2016 zikisomwa pamoja na Kifungu cha 28B (1)(a) cha Sheria ya Kuzuia Utakasishaji wa Fedha Haramu, Na. 12 ya Mwaka 2006.

Mganga ameeleza kuwa Septemba 05, 2020 Jeshi la Polisi Tanzania lilimkamata Kubenea akiwa katika gari la abiria lenye namba ya usajili T 645 DKR akitokea kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya, eneo la Namanga akielekea Arusha mjini.

Taarifa hiyo inasema kuwa mara baada ya upekuzi, mtuhumiwa huyo alikutwa, pamoja na vitu vingine, Dola za Marekani *USD* 8,000 (zaidi ya Tsh milioni 18), Shilingi za Kenya 491,700 (zaidi ya Tsh milioni 10), pamoja na Shilingi taslimu za Kitanzania 71,000.

Pia baada ya mwanasiasa huyo kupekuliwa, taarifa inaeleza kuwa alikutwa na tiketi ya basi la Super Couch lenye namba ya usajili KCP 4230 ya Septemba 05, 2020 kutoka Nairobi, Kenya kwenda Namanga.

“Pia alikutwa na ‘Memorandum of Understanding kati ya Hali – Halisi (Tanzania), Buni Media Limited (Kenya), Risiti ya malipo ya hoteli itwayo After 40 Hotels Limited iliyopo Nairobi, Kenya yenye jina la Kubenea, Saed Ahmed kama mgeni kuanzia Septemba 3,2020 hadi Septemba 5,2020 na pasi ya kusafiria,”ilieleza taarifa hiyo.

Aidha mara baada ya kukamatwa, Kubenea alieleza kuwa alifika mkoani Arusha mnamo Septemba 02, 2020 akitokea Dar es Salaam na kufikia katika hoteli iliyopo Arusha mjini. Alieleza zaidi kuwa, Septemba 03, 2020 alienda kulala kwa kaka na kisha Septemba 04, 2020 alienda Namanga na kupokea fedha taslimu tajwa hapo juu kutoka kwa raia wa Kenya.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mashtaka alieleza kupitia taarifa hiyo kuwa mara baada ya kupitia ushahidi uliokusanywa alibaini kuwa; Kubenea hakufikia katika hoteli aliyoitaja Arusha mjini, wala kulala kwa Kaka yake kama alivyoeleza.

Chanzo: habarileo.co.tz