Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kubenea ataka TCRA itoe taarifa kuhusu udukuaji

67825 Pic+kubenea

Mon, 22 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano nchini (TCRA) kutoa taarifa za waliohusika kudukua mawasiliano ya simu ya mbunge wa Mtama, Nape Nnauye na watu wengine.

Hivi karibuni, sauti fupi za mazungumzo ya simu yanayomhusisha Nape, aliyekuwa Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba na makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii

Akizungumza na vyombo vya habari leo Julai 22, Kubenea amesema kitendo kilichofanyika ni kinyume cha katiba na sheria za nchi ambazo zinatoa uhuru wa faragha kwa mtu.

"Haya mambo hayawezi kufanyika katika nchi inayojali utu wa mtu. TCRA itoe taarifa, ni nani aliyefanya kazi hiyo chafu.

"Nchi hii ina mabalozi wa nchi mbalimbali, sasa kama Nape na Kinana wamerekodiwa, nani anajua kwamba mabalozi hawajarekodiwa? TCRA na vyombo vyote vya ulinzi na usalama vieleze ni nani anayefanya kazi hiyo ya kurekodi watu," amesema Kubenea.

Mbunge huyo amewataka Watanzania kutokubali kutukanwa na kuondolewa utu wao na watu wanaoingilia faragha zao kwa sababu ni kosa la jinai.

Pia Soma

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Suzan Lyimo ambaye aliambatana na Kubenea, amesema Ibara ya 16 ya Katiba ya Tanzania inaeleza wazi kwamba kila mwananchi ana haki ya faragha yake ambayo inatakiwa kuheshimiwa na watu wote.

"Hili la kudukuwa mawasiliano linaweza kufanywa na vyombo vya usalama kwa watu ambao wanahatarisha amani na usalama wa nchi. Sidhani kama hizi tunazozisikia zinahatarisha amani," amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz