Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kortini kwa kumiliki kobe 116

Kobeee Kortini kwa kumiliki kobe 116

Wed, 21 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Raia wa Ukraine, Orga Kryshtopa amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashtaka mawili ya kujihusisha na kumiliki nyara za serikali kinyume cha sheria.

Orga anashitakiwa kwa kumiliki kobe 116 wenye thamani ya Sh 18,935,840 na alisomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Judith Kyamba mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Amir Msumi.

Kyamba alidai kuwa kati ya Januari Mosi na Julai 30, 2022 mkoani Dar es Salaam, Orga alijihusisha na nyara za serikali kwa kununua, kuuza na kusafirisha kobe 116 mali ya serikali bila kibali kutoka katika mamlaka husika.

Katika shitaka la pili, Kyamba amedai katika tarehe tajwa eneo la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Dar es Salaam, Orga alikamatwa akiwa na kobe 116 bila ya kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo. Aidha, ilidaiwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika. Iliahirishwa hadi Juni 28, mwaka huu.

Kyamba aliieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na upande wa mashitaka unatarajiwa kuongeza mshitakiwa mwingine.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live