Wakazi wawili wa Dar es Salaam wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya kukutwa na vipande 19 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh milioni 175.8.
Washitakiwa hao ni Fadhil Saidi (44) mkulima na mkazi wa Kiwalani na Daniel Ndunguru (35) mjasiriamali na mkazi wa Tandika.
Akisoma mashitaka hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate, Wakili wa Serikali, Yusuph Aboud alidai kuwa washitakiwa walitenda kosa hilo Mei 3, mwaka huu maeneo ya Ukonga Sabasaba, Dar es Salaam.
Alidai washitakiwa kwa pamoja walikutwa na vipande 19 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Marekani 750,000 sawa na Sh 175,875,000 bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote na upande wa mashitaka ulidai upelelezi wa shauri hilo unaendelea hivyo aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo, wakili wa utetezi, Steven Mbwana alidai sheria mpya ya uhujumu uchumi inaipa mahakama mamlaka ya kutoa dhamana iwapo thamani ya fedha haijazidi Sh milioni 300 hivyo aliomba washitakiwa wapatiwe dhamana.
Hakimu Kabate alimtaka kila mshitakiwa kuwa na fedha taslimu au kuwasilisha hati ya mali yenye thamani ya Sh 43,968,750.
Pia aliwataka kuwa na wadhamini wawili kila mmoja watakaosaini bondi ya Sh milioni mbili sambamba na kuwa na utambulisho kutoka taasisi au sehemu anayofanyia kazi.
Washitakiwa hao pia wametakiwa kuwasilisha mahakamani hapo hati zao za kusafiria na kwamba hawataruhusiwa kutoka nje ya mamlaka hiyo bila kuwa na kibali cha mahakama.
Washitakiwa wamerudishwa rumande hadi Juni 9, mwaka huu kwa sababu ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.