Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kortini akidaiwa kumzushia Rais Magufuli uongo

38181 Uongo+pic Kortini akidaiwa kumzushia Rais Magufuli uongo

Thu, 24 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mfanyabiashara, Henry Munis (30) mkazi wa Mbeya amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka moja la kuchapisha taarifa za uongo dhidi ya Rais John Magufuli na kuzisambaza katika mtandao wa kijamii wa facebook.

Munis alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa shtaka hilo na wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita mbele ya hakimu mkazi, Salum Ally.

Akisoma hati ya mashtaka, wakili Mwita alidai kuwa Desemba 28 mwaka jana katika maeneo ya Veta jijini Mbeya, mshtakiwa alichapisha taarifa katika ukurasa wake wa facebook akiandika: ‘Jinsi Magufuli alivyochota trilioni 1.5 za ATCL (Shirika la Ndege Tanzania) akitumia ujanja wa kuleta ndege ili atuibie’, huku akijua taarifa hizo ni za uongo na zenye nia ya kuupotosha umma.

Hata hiyo mshtakiwa huyo alikana kutenda kosa hilo.

Wakili wa utetezi, Hekima Mwasipu aliiomba Mahakama kumpatia mshtakiwa huyo dhamana kwa kuwa shtaka hilo linadhaminika.

Akitoa masharti ya dhamana, hakimu Ally alimtaka Munisi kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho na picha zao ambao pia watasaini bondi ya Sh500,000 kila mmoja. Mshitakiwa alitimiza masharti hayo na yuko nje kwa dhamana.

Mahakama pia ilimtaka ahudhurie mahakamani hapo kila tarehe inapopangwa kesi hiyo.

Baada ya kusomwa hati ya mashtaka, upande wa mashtaka ulieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kwamba wanaendelea kukamilisha baadhi ya vitu vilivyosalia.

Hakimu Ally aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 6 itakapotajwa tena.



Chanzo: mwananchi.co.tz