Athuman Mohamed (44), mkazi wa Mbagala Mission, amefikishwa leo katika mahakama ya Wilaya ya Temeke, akishtakiwa kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa gramu 55.
Akisoma hati ya mashtaka, Mwendesha Mashitaka katika mahakama hiyo, Rockus Komba, amesema mtuhumiwa alikamatwa akiwauzia bangi wateja wake nyumbani kwake Mbagala Mission mnamo Januari 3, 2023.
"Mtuhumiwa alikamatwa na Afande Rajabu na wenzake waliokuwa katika doria, walimkuta nyumbani kwake pamoja na vijana aliokuwa akiwauzia bangi ambao walitoroka baada ya polisi kufika.
Polisi walipokagua nyumba yake walimkuta na puli moja alilolificha chini ya kitanda," amesema mwendesha mashtaka huyo.
Komba amesema sampuli iliyopelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, ilithibitishwa kuwa dawa ya hizo za kulevya ni aina ya bangi (cannabis sativa) na kwamba zina uzito wa gramu 55.
Hata hivyo, mtuhumiwa amekana maelezo yaliyotolewa na kudai kwamba yeye ni mvutaji, si muuzaji au msafirishaji kama inavyodaiwa.
"Mheshimiwa mimi si muuzaji, ninavuta kutokana na kazi zangu ninazofanya. Huwa nanunua kiasi cha kunitosha kuvuta kwa siku kadhaa," alidai Athuman.
Hakimu ameahirisha shauri hilo mpaka Septemba 29, 2023; mahakama itakapowasikiliza mashahidi kutoka upande wa Jamhuri wanaotarajia kuwa watano.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi, John Ngeka inahusu usafirishaji wa dawa za kulevya kinyume na kifungu 15A (1), (2), (c) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya namba 95 marejeo ya mwaka 2019.