Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kortini akidaiwa, kughushi, ‘kutumbua’ pesa za marehemu baba yake

Nyundoo Kortini akidaiwa, kughushi, ‘kutumbua’ pesa za marehemu baba yake

Wed, 26 Jul 2023 Chanzo: Mwananchi

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inatarajia kusikiliza mashahidi zaidi ya kumi pamoja na vielelezo saba katika kesi inayomkabili Samweli Gombo na Musa Yohana, ambao wanakabiliwa na shtaka la kughushi cheti cha kifo na wizi wa zaidi ya Sh102 milioni.

Wakili wa Serikali, Mosie Kaima, ameyasema hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemalira, wakati kesi hiyo ilipoletwa kwa ajili ya kuwasomea hoja za awali washtakiwa hao.

Mosie alidai kwamba mshtakiwa huyo (Samweli) anakabiliwa na shitaka la wizi, kughushi cheti cha kifo cha marehemu baba yake Stanford Gombo, kughushi nyaraka ya nguvu ya kisheria na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, huku mshitakiwa Yohana akiwa na shitaka moja la kughushi.

Inadaiwa kwamba mshtakiwa Samweli alifiwa na baba yake mzazi ambaye ni Stanford Gombo Novemba 11, 2017; na kuzikwa Novemba 13 mwaka huo, ambapo aliacha mali mbalimbali ikiwemo fedha Sh102, 900,784 katika benki ya NMB.

Imedaiwa kuwa mwaka 2019 familia ya Stanford ilikaa kikao cha familia na kumteua Yaredi Gombo kuwa msimamizi wa mirathi.

Mosie amedai kuwa mshtakiwa Samweli alibaki na kadi ya ATM ya marehemu baba yake na hakutaka kusema licha ya wanafamilia kuitafuta kadi hiyo.

Wakili huyo wa Serikali aliendelea kudai kuwa mshtakiwa alichukua fedha kutoka katika akaunti hiyo katika tarehe tofauti kati ya Novemba 13 207 hadi Juni 30 2018 na kufikia jumla ya kiasi hicho cha fedha.

Ilielezwa kuwa mshtakiwa huyo alighushi cheti cha kifo cha baba yake akidai kuwa kimetolewa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), pia alighushi muhtasari wa kikao cha familia na nyaraka ya nguvu ya kisheria na kuwasilisha katika mahakama ya mwanzo ya Chakwale wilayani Gairo.

Ilidaiwa kwamba washtakiwa hao walikamatwa na kufikishwa mahakamani Mei 6, 2022.

Baada ya kusomwa mashtaka hayo mshtakiwa alikiri baba yake kuacha fedha hizo, kubaki na kadi ya benki ya baba yake na pia alikiri kuchukua fedha hizo huku mshitakiwa Yohana akikana maelezo hayo isipokuwa majina yake na anuani.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 9, 2023 kwa ajili ya kusikilizwa.

Chanzo: Mwananchi