Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kortini akidaiwa kuchapisha taarifa za uongo facebook

41862 FB+PIC Kortini akidaiwa kuchapisha taarifa za uongo facebook

Fri, 15 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Emmanuel Mahumbi mkazi wa jiji la Mwanza  (38) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa kijamii wa facebook.

Akisoma hati ya mashtaka leo Alhamisi Februari 14, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando, wakili wa Serikali Ester Martin amedai Septemba 2018 katika Jiji la Dodoma Mahumbi alichapisha taarifa za uongo katika mtandao wa facebook zikisema:

"Kichaa m1 anatoa kafara kiboya kweli kaenda kumuona dada yake Bugando kumbe ndio anaenda kumkabidhi Freemason cku moja 2 baada ya kukuona akafa na kufa 2/ kaenda kuwatembelea Ukerewe cku 2 tu baada ya kuwaona wakafa na kufa kumbe alienda kuwakabidhi kwa freemason boya kweli mwambieni abadilike atamaliza watu".

Wakili Ester amedai taarifa hizo ni za uongo na zingeweza kusababisha chuki katika jamii.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa alikana na wakili Ester alieleza kuwa upelelezi haujakamilika.

Wakili wa utetezi Hekima Mwasipu, ameiomba Mahakama kumpatia mshtakiwa dhamana kwa kuwa kosa aliloshtakiwa nalo linadhaminika.

Akitoa masharti ya dhamana, Hakimu Mmbando amemtaka mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua kutoka taasisi inayotambulika na watakaosaini hati yenye thamani ya Sh10 milion kila mmoja.

Mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kupelekwa rumande hadi Februari 28, 2019 itakapotajwa tena.



Chanzo: mwananchi.co.tz