Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Korti yakubali mshtakiwa mauaji ya mkewe kupimwa afya ya akili

MAUAJI MKEWE Korti yakubali mshtakiwa mauaji ya mkewe kupimwa afya ya akili

Fri, 8 Sep 2023 Chanzo: mwanachidigital

Upande wa utetezi katika kesi inayomkabili Hamis Luoga anayekabiliwa na shtaka la mauaji ya mkewe, Naomi Marijani umeiomba Mahakama mshtakiwa huyo akapimwe afya ya akili.

Wakili wa utetezi, Mohamed Majaliwa ameiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, mshtakiwa apelekwe Hospitali ya Isanga mkoani Dodoma akapimwe afya ya akili kabla ya kuendelea na shauri hilo. Mahakama imekubali ombi hilo.

Luoga anadaiwa kumuua Naomi, kuuchoma moto mwili wake kwa kutumia magunia mawili ya mkaa na majivu yake alikwenda kuyafukia shambani kwake.

Wakili wa utetezi Majaliwa anayeshirikiana na Michael Kibindo, aliwasilisha ombi hilo jana mbele ya Jaji Mussa Pomo, shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa hoja za awali. Majaliwa alisema wanaomba mshtakiwa akafanyiwe uchunguzi kwa kuwa wana wasiwasi, kwani hata wanapozungumza naye hayupo sawa kiakili.

Alidai hawawezi kusikiliza mashahidi hadi hospitali itakapotoa majibu ya uchunguzi wa afya ya akili ya mshtakiwa na Jaji Pomo alikubali ombi hilo. Alisema shauri hilo litapangiwa tarehe baada ya majibu ya hospitali.

Awali, Wakili wa Serikali Dorothy Masawe alidai wanatarajia kusikiliza mashahidi 28 na watakuwa na vielelezo 15 katika kesi hiyo. Akimsomea mshtakiwa hoja za awali alidai kati ya vielelezo hivyo, saba ni vya nyaraka na vinane ni vitu halisi.

Alidai Mei 15, 2019 eneo la Gezaulole wilayani Kigamboni mshtakiwa alimuua kwa kukusudia Naomi.

Mshtakiwa anadaiwa Mei 19, 2019 aliripoti kituo cha polisi cha Mji Mwema kuwa mkewe Naomi na mwanaye wametoweka tangu Mei 17, 2019.

Inadaiwa alipohojiwa na polisi kituoni alikiri kumshambulia mkewe hadi kufa, baadaye alichukua mwili na kuupeleka kwenye kibanda na kuuchoma kwa mkaa.

Mshtakiwa anadaiwa katika mahojiano hayo, alieleza baada ya kuuchoma mwili alichukua mabaki ya majivu na kuyaweka kwenye mfuko. Kwa kutumia gari lake aina ya Subaru Forester aliyabeba na kuyapeleka shambani kwake eneo la Mlogolo wilayani Mkuranga mkoani Pwani.

Wakili Massawe alidai katika mahojiano hayo mshtakiwa anadai alichimba shimo kwenye shamba lake na kuyafukia. Pia alipanda mgomba juu yake.

Baada ya maelezo hayo anadai vilichukuliwa vinasaba vya majivu kwenda kupimwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, ndipo ilipobainika kuwa yalikuwa mabaki ya mwili wa Naomi.

Chanzo: mwanachidigital