Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kizimbani kwa tuhuma za kusafirisha binadamu

Wed, 9 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mfanyabiashara, Abdallah Siminda(30)  maarufu Maniga  amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu shtaka la kusafirisha binadamu.

Siminda ambaye ni mkazi wa Tanga eneo la Mabawa, amepandishwa kizimbani leo Januari 7, 2019 kujibu shtaka linalomkabili.

Akisoma hati ya mashtaka wakili wa Serikali, Neema Mbwana amedai mbele ya Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando kuwa mshtakiwa anadaiwa kusafirisha binadamu kinyume cha sheria.

Mbwana amedai mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Desemba Mosi na 13, 2018 eneo la Boko Chama, wilaya ya Kinondoni.

Amedai siku hiyo ya tukio mshitakiwa alimchukua Ashura Kassimu na kumpeleka kufanya kazi za ndani kama bondi la deni alilokuwa anadaiwa sehemu hiyo.

Mshitakiwa baada ya kusomewa shtaka linalomkabili, alikana kutenda kosa na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

“Upelelezi wa kesi hii bado haujakamilika, hivyo tunaomba terehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amedai wakili Mbwana.

Hakimu Mmbando ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 21, 2019.

Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka linalomkabili kutokuwa na dhamana.



Chanzo: mwananchi.co.tz