Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kizimbani kwa tuhuma za kuiba mabaki ya madini

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watuhumiwa saba wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu ikiwemo wizi wa mapipa 20 ya mabaki ya madini yenye thamani ya zaidi ya Sh900 milioni.

Washitakiwa hao wamefikishwa mahakamani leo Jumanne Machi 26, 2019 na kusomewa mashtaka hayo na wakili wa Serikali,  Jenifa Masue mbele ya hakimu mkazi, Agustino Mmbando.

Washtakiwa hao ni Jacob Kihombo, Yahya Masoud, Mbaraka Lipinda, Ramadhan Zombe, Waziri Kibua, Mustapha Mnyika na Richard Sangana.

Akisoma mashitaka hayo wakili Masue amedai washtakiwa walitenda makosa hayo kati Februari 6 na 7, 2019 jijini Dar es Salaam.

Katika shtaka la kwanza, Masue amedai washtakiwa wote walitenda kosa la kula njama ya wizi wa mali inayosafirishwa.

Katika shitaka la pili amedai katika tarehe hizo washitakiwa wote waliiba mapipa 20 ya mabaki ya madini aina ya Tantalite Concentrates yenye thamani ya Sh938,339,907 mali ya kampuni ya Bollore Transport and Logistics.

Katika shtaka la tatu linalomkabili mtuhumiwa wa nne, Zombe ambaye ni mlinzi, anadaiwa katika tarehe hizo akiwa mwajiriwa wa kampuni ya Bollore, alishindwa kuzuia kutendeka kwa kosa la wizi wa mapipa hayo ya madini.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washitakiwa wote walikana na upande wa mashtaka umedai upelelezi haujakamilika.

Akitoa masharti ya dhamana Hakimu Mmbando alimtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua na vitambulisho kutoka taasisi ya umma na kuwasilisha mahakamani hapo hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh52milioni.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 9, 2019 kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa wote walirudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana .

 



Chanzo: mwananchi.co.tz