Dar es Salaam. Wakazi wawili wa mkoani Morogoro wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matano ya kukutwa na nyara za Serikali, ukiwemo ubongo wa fisi.
Wakili wa Serikali Tully Helela amewataja washtakiwa hao kuwa ni Salum Kaluona (65) na Juma Kigombalima (43).
Akiwasomea mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi, Augustina Mmbando leo Alhamisi Agosti Mosi, 2019, Helela amedai washtakiwa hao wametenda kosa hilo Julai 11, 2019 eneo la Buguruni, Dar es Salaam.
Amesema wamekutwa na nyara hizo zenye thamani ya Sh27.2milioni.
Katika shtaka la kwanza, Helela amedai siku na eneo hilo, washtakiwa walikutwa na mikia mitano ya nyumbu, shtaka la pili ni kukutwa na pua mbili, mikia miwili na ubongo wa fisi.
Iliendelea kudaiwa mahakamani hapo kuwa katika shtaka la tatu, siku na eneo hilo la Buguruni, washtakiwa walikutwa na koromeo moja na kipande kimoja cha ngozi ya simba.
Pia Soma
- Wahofia kuondolewa kwenye maeneo ya kufanyia biashara
- Rais John Magufuli kuzindua Terminal 3 muda mfupi ujao
- Uhamiaji Tanzania yachukua paspoti saba nyumbani kwa Kabendera
- Serikali ya Tanzania yasaini mkataba ujenzi barabara ya lami Tanga - Pangani
Hata hivyo, upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi bado haujakamilia na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kesi hiyo kutajwa.
Hakimu Mmbando ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 13, 2019 huku washtakiwa wakirudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.