Dar es Salaam. David Ramadhani Iddy (33) mkazi wa Tabata Segerea amefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Kinondoni kwa kosa la kujifanya ofisa wa Jeshi la Polisi na la Kujenga Taifa (JKT).
Wakili wa Serikali, Asp Hamisi amesema mbele ya hakimu, Joyce Mushi kuwa mshtakiwa anakabiliwa na makosa mawili.
Amesema Julai 19, 2019 mshtakiwa alijifanya ofisa wa jeshi hilo na kosa la pili ni kukutwa na vifaa vya umma kinyume na sheria.
Hamisi amesema katika shtaka la kwanza mshtakiwa alijifanya ofisi wa JKT kama msimamizi msaidizi kwa kuvaa sare za jeshi hilo akijua si halali na alikutwa eneo la JKT Makao Makuu Mlalakuwa, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Katika shtaka la pili, Hamisi amedai mshtakiwa alikutwa na sare za polisi, sare moja ya kijani, nyota za vyeo mbalimbali za polisi, begi moja, kofia moja, mikanda mitatu, kofia moja ya ofisa usalama wa polisi, buti, pingu, redio call na pea moja ya sare za Tunica kinyume na sheria.
Mshtakiwa huyo alikana shtaka hilo na kudai amesingiziwa huku wakili Hamisi akieleza kuwa upelelezi unaendelea.
Pia Soma
- Upande wa utetezi kutumia video kumhoji shahidi kesi ya kina Mbowe
- Makonda ataka usafi Dar kuendelea kama ilivyokuwa katika mkutano Sadc
- Ripoti yawataja wenye ualbino kuishi kwa wasiwasi kuelekea uchaguzi
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 2, 2019.