Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kizimbani akidaiwa kuvunja, kuiba simu kituo cha Polisi

Hukumu Pc Data Kizimbani akidaiwa kuvunja, kuiba simu kituo cha Polisi

Wed, 23 Aug 2023 Chanzo: mwanachidigital

Mbeba mizigo ‘kibega’ katika soko la Mbuyuni mjini Moshi, Jackson Mussa (20), amepandishwa kizimbani akituhumiwa kuvunja kituo cha kati cha Polisi Moshi na kuiba vielelezo mbalimbali.

Katika kesi hiyo namba 151 ya 2023 iliyofungulia katika Mahakama ya Wilaya ya Moshi, Mussa ameunganishwa na watuhumiwa wengine watano wanaotuhumiwa kukutwa na vitu vilivyoibwa katika kituo hicho cha polisi.

Watuhumiwa hao ambao wako nje kwa dhamana baada ya kukana mashtaka isipokuwa Jackson Mussa ni Bakari Ibrahim (27), Charles Mmbaga (29) na Juma Mudathiri (27) wakazi wa Njoro Railway na Swalehe Abdalah (29) mfanyabiashara mkazi wa Pasua.

Pia ameunganishwa Stella Oscar (24) ambaye ni Stasheni Masta wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) katika stesheni kuu ya Moshi iliyopo eneo la Njoro Railway katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Watuhumiwa hao walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi, Rehema Olambo na kusomewa mashtaka na wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, kanda ya Moshi, Agatha Pima na kesi itaanza kusikilizwa Agosti 28, mwaka huu.

Mashtaka ya kuvunja kituo

Shitaka la kwanza, wakili Agatha alidai Aprili 10, 2023 usiku katika kituo cha kati Moshi, Jackson alivunja na kuingia kituo hicho kwa nia ya kutenda kosa na kisha kuiba simu aina ya Infinix Hot 10i, Samsung A03 Core, Infinix Smart HD, Samsung note 20, Tablet ZTE T1002 na kompyuta mpakato aina ya Lenovo.

Vitu hivyo vilikuwa katika chumba cha kuhifadhi vielelezo, mali ya kituo cha kati cha Polisi Moshi.

Katika shtaka la tatu, ilidaiwa Aprili 28, 2023 katika kituo kati cha Polisi Moshi, mshtakiwa alipatikana na simu aina ya Infinix na Tablet namba T1002 AU akijua au akiamini vitu viliibwa au kupatikana kwa njia isiyo halali.

Katka shtaka la nne, mshtakiwa Bakari Hassan anadaiwa Aprili 25, 2023 akiwa kituo cha kati cha Polisi alipatikana na simu aina ya Infinix Hot 10 inayodhaniwa ni mali ya wizi.

Shtaka la tano linamhusu mshtakiwa Charles Mmbaga anayedaiwa Mei mosi, 2023 huko Railway Njoro alimpatia Stella Oscar simu Samsung Note 20 Ultra inayoaminika kuwa ni mali ya wizi.

Katika shtaka la sita, inadaiwa Aprili 26, 2023 mshtakiwa Juma Mudathiri alipatikana na simu aina ya Samsung A03 Core huku akijua au akiamini ni ya wizi.

Katika shtaka lingine, Swalehe Madafi anadaiwa Aprili 25, 2023 eneo la Umoja wa Vijana, alipatikana na kompyuta mpakato aina ya Lenovo na chaji yake huku Stella Oscar akidaiwa Aprili mosi, 2023 eneo la Railway Njoro alipatikana na simu aina ya Samsung Note 20 akijua ni mali ya wizi.

Chanzo: mwanachidigital