Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kivuli cha mauaji ya wanawake chaendelea kutisha wananchi Mto wa Mbu

44751 Pic+wanawake Kivuli cha mauaji ya wanawake chaendelea kutisha wananchi Mto wa Mbu

Tue, 5 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wanawake wa mji wa Mto wa Mbu, wilayani Monduli Mkoa wa Arusha, bado wana hofu ya kuuawa kutokana na mauaji yanayofanana ya wanawake tisa wa mji huo.

Katika mji huo uliopo takribani kilomita 100 kutoka Arusha mjini, shughuli kubwa ya wakazi wake ni kilimo cha ndizi na biashara.

Mto wa Mbu ambayo inapakana na wilaya ya Karatu, pia ni moja ya miji ya kitalii kwa kuwa ipo katika njia kuu inayopitwa na watalii wengi kwenda hifadhi za Manyara, Serengeti na Ngorongoro hivyo kufanya baadhi yao wakati mwingine kuweka kambi hapo.

Wakizungumza na mwananchi mjini humo, baadhi ya wananchi, walieleza kuwa bila ya jeshi la polisi na jamii kudhibiti matukio hayo mauaji kama yale yaliyofanyika kwa wanawake tisa yataendelea.

Mchungaji kiongozi wa Kanisa la Elim Mto wa Mbu, Philip Fisso ambaye mtoto wake alibakwa kisha kuuawa, Februari 4, mwaka huu, alisema ni muhimu polisi na jamii kushirikiana, kudhibiti matukio hayo. Mchungaji Fisso analisema hilo baada ya binti yake, Ester Fisso (26) mama wa watoto wawili kuwa mmoja wa wanawake tisa waliouawa.

Anasema nyuma ya mauaji hayo yapo mambo mengi yanayotajwa ikiwamo ushirikina ingawa hilo haliwezi kuthibitishwa bayana. Pia, anaamini ulevi ni tatizo lingine linalopaswa kutazamwa kwa karibu.

Mchungaji Fisso anasema, katika mji huo na maeneo ya jirani, kuna vilabu vingi vya pombe ambavyo hufunguliwa kwa saa 24 jambo ambalo ni hatari.

“Vijana wengi wanatumia muda wao katika ulevi, hivyo nadhani Serikali inapaswa kusimamia sheria ya kuzuia ulevi hasa mchana,” anasema.

Anasema binti yake kabla ya kuuawa alifanyiwa ukatili na wauaji hao.

“Siku ya tukio alituaga anatoka na rafiki yake wa kiume ambaye walipanga kufunga ndoa karibuni, lakini hakurudi na asubuhi tulipata taarifa ya mwili wake kuokotwa,” anasema. Mwili ya Ester ulipatikana katika eneo la Comwex katika mji huo.

Doto Elias, ambaye dada yake, Ruth Alias aliuawa mwaka jana, anasema ni muhimu wanaofanya unyama huo wakajulikana na kuchukuliwa hatua.

“Sisi kama familia hadi sasa hatuwajui wahusika, tumeamua kumwachia Mungu na kila siku tunaomba wapatikane,” anasema. Akiungana na wenzake, mkazi mwingine wa mji huo, Ally Salimu anayeishi katika eneo la Kigongoni Mto wa Mbu, anasema anaamini chanzo cha mauaji ya wanawake ni ushirikina kwani wanauliwa bila kuibiwa chochote.

“Ingekuwa wanachukuliwa mali tungesema ni vibaka, lakini hawachukuliwi kitu, wanabakwa na kufanyiwa ukatili mkubwa kisha wanatupwa,” anasema.

Mmoja wa manusura wa tukio linalohusishwa na mauaji ya wanawake katika mji huo, Fatuma Adam (84) ambaye alinusurika kuuawa baada ya kufanyiwa ukatili, anasema Septemba, mwaka jana, akiwa anakusanya kuni aliwaona vijana watatu wakiwa wamevaa nguo nyeusi.

Anasema vijana hao walianza kumfuata bila kujua lengo lao na ghafla walimvamia “nilipiga kelele bila mafanikio, nakumbuka ilikuwa kama saa 12 jioni hivi na baada ya hapo nilipoteza fahamu”.

Anasema alipata fahamu akiwa hospitalini akipatiwa matibabu na mpaka sasa bado hali yake kiafya haijatengemaa.

“Naomba Serikali isaidie kuwasaka wahusika. Nadhani ni ushirikina maana bibi kama mimi mtu mwenye akili timamu hawezi kunifanyia mambo mabaya,” anasema.

Kikosi cha intellijensia chaanza kazi

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Longinus Tibishubwamu anasema jeshi hilo limeshapeleka kikosi cha intellijensia katika mji huo kuhakikisha mtandao wa watu wanaoteleza hualifu huo unapatikana na kukomeshwa.

Anasema tayari wanazo taarifa wanazifanyia kazi kuhusiana na matukio hayo kujua kama yanafanyika kwa imani za kishirikina au ni ulevi.

“Ule mji unamakabila mengi sana, sasa tunachunguza kila taarifa na hata waganga wa kienyeji ambao wamekuwa wakipiga ramli chonganishi tutawabaini,” anasema.

Anasema kwa tukio la kifo cha mtoto wa mchungaji, Philip Fisoo polisi wanamshikilia mpenzi wake ambaye alikuwa naye siku ya tukio.

“Mto wa Mbu kuna biashara kubwa ya pombe ya gongo tutafuatilia na tutadhibiti unywaji wa pombe kwani unachangia uhalifu,” anasema.

Mbali na Ester wanawake wengine wanane waliouawa na kutambulika ni Ruth Elias, Vick Kivuyo, Elizaberth Hango, Shikweshi Boaz, Mwapwani Mawezo na Khadija Raphael.

Uchunguzi wa kitabibu

Uchunguzi wa kitabu ulionyesha wanawake wote waliouawa katika matukio hayo, waliuawa baada ya kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji.

Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Kigongoni jirani na eneo la Mto wa Mbu, Dk Emma Msofe anasema matukio yote ya mauaji yanafanana kwani waathirika walifanyiwa ukatili wa kijinsia.

Hata hivyo, Dk Msofe anasema kwa sababu za kitabibu na maagizo ya Serikali hawezi kufafanua zaidi juu ya uchunguzi wa mauaji hayo kwani suala hilo bado linachungzwa kwa kina na vyombovya dola.

Wanawake wazee kutunzwa

Kutokana na tishio la usalama kwa wazee hasa wanawake katika mji huo, Jackline Samson ambaye ni mdau wa maendeleo na mkazi wa mji huo kwa kushirikiana na marafiki zake wameanzisha shirika la Uzee na Furaha linalolenga kusaidia mapambano dhidi ya matukio hayo.

Jackline ambaye ndiye mkurugenzi wa shirika hilo, anasema wanawake hasa wazee wasiojiweza wamekuwa wahanga wa matukio ya udhalilishaji. “Ingawa bado tunatafuta wafadhili zaidi, lakini tumejenga kituo ambacho kinaweza kuwakutanisha na kuwapa hifadhi ili waishi kwa furaha,” anasema.

Anasema pia wameanza kutoa huduma za afya, chakula na mahitaji mengine kwa wazee majumbani.

Hata hivyo, anasema ni muhimu jamii na vyombo vya dola kushirikiana kuhakikisha watuhumiwa wanakamatwa.

“Nnaamini wahusika wapo hapa ni watoto wa hapa hapa, ili wakamatwe lazima wazazi na jamii tushirikiane,” anasema.

Ofisa ustawi wa jamii tarafa ya Manyara, Swedi Kiluvia anasema matukio ya udhalilishaji wanawake yamekuwa tishio kubwa katika mji wao.

“Tunaimani Serikali itayakomesha kwani tayari kuna dhamira inayooneshwa ili kuwakamata wahusika wote,” anasema.

Hata hivyo, aliikumbusha jamii katika mji huo kuishi kwa kufuata maadili mema, kuwaheshimu kinamama, wazee wanawake na kujiepusha na matukio ya kihalifu.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola akiwa katika ziara mkoani Arusha hivi karibuni, alipokea malalamiko ya wananchi juu ya mauaji hayo.

Waziri Lugola alisema haiwezekani Serikali ya Rais John Magufuli kukubali kuendelea kwa mauaji katika mji huo na kuwakosesha amani na utulivu wananchi.

“RPC leta hapa kikosi cha intellijenjia wakae hapa kuhakikisha wanakusanya taarifa za wahalifu na kuwakamata,” alisema Lugola alipozungumza na wananchi katika mji huo.



Chanzo: mwananchi.co.tz