Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kitanzi palepale waliomuua RPC

Waliomuuapiic Data Kitanzi palepale waliomuua RPC

Sat, 13 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jopo la majaji watatu wa mahakama ya Rufani Tanzania limebariki adhabu ya kifo iliyotolewa Novemba 2019 kwa washitakiwa wanne, waliotuhumiwa kumuua kwa kumpiga risasi aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow.

Katika hukumu hiyo iliyosomwa juzi jijini Mwanza na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Emmanuel Mrangu, majaji hao; Mwanaisha Kwariko, Dk Marry Levira na Abraham Mwampashi, wamebariki watu hao wanyongwe hadi kufa.

Muganyizi Michael, Magige Marwa, Abdalah Petro na Abdulrahman Athman, walihukumiwa adhabu hiyo Novemba 12, 2019 na Jaji Sirialus Matupa, lakini wakakata rufaa kupinga kutiwa hatiani na pia adhabu waliyopewa.

Wakirejea ushahidi uliowatia hatiani, majaji hao walisema usiku wa Oktoba 13, 2012 huko eneo la Kitangiri katika wilaya ya Ilemela, washitakiwa walimuua kwa makusudi kwa kumpiga risasi Barlow.

Kulingana na ushahidi huo, siku hiyo marehemu na shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka, Dorothy Moses, walikuwa wamerejea kutoka kikao cha harusi na walikuwa nje ya lango kuu la nyumba anayoishi Dorothy, wakisubiri kufunguliwa.

Wakiwa bado wako kwenye gari ya marehemu aina ya Toyota Hilux Pick-Up namba T779 BFY, walivamiwa na watu watano, na wawili kati yao walimfuata kamanda huyo na kujitambulisha kwao kuwa wao walikuwa ni askari polisi.

Walimhoji kwa nini alikuwa amewamulika na hapo Barlow alijitambulisha kuwa yeye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza na kuwahoji walikuwa ni askari wa wapi na hapo ndipo mmoja wao alipomfyatulia risasi na kufa papo hapo.

Baada ya kumuua, walichukua simu ya upepo (radio call) na funguo za gari na pia wakampora simu ya kiganjani ambayo katika ufuatiliaji ilikutwa kwa shahidi wa pili wa upande wa mashitaka, aliyeeleza kuuziwa na mrufani wa kwanza, Michael.

Upande wa mashitaka uliita mashahidi 25 na kuwasilisha vielelezo 35 ambavyo Jaji Matupa aliegemea kutoa hukumu yake na kusema ushahidi dhidi ya washitakiwa haukuacha mashaka kuwa wao ndio waliomuua Barlow.

Rufaa yao ilivyokuwa

Kupitia kwa mawakili Anthony Nasimire, Constantine Mutalemwa, Deocles Rutahindurwa na Cosmas Tuthuru, washitakiwa walikata rufaa wakiiomba mahakama kufuta kutiwa hatiani na adhabu ya kifo waliyopewa wateja wao.

Kiujumla katika rufaa hiyo, washitakiwa waliegemea sababu kuwa kutiwa kwao hatiani kuliegemea hitimisho batili la kisheria na ushahidi ambao haukuunganika katika utambuzi wa washitakiwa, maelezo ya ungamo na alama za vidole. Katika hukumu yao iliyosomwa Jumatatu Agosti 9, 2011 na nakala yake kupatikana jana, majaji hao watatu walitupilia hoja hizo na kukubaliana na upande wa Jamhuri na kwamba ushahidi uliunganisha na mashitaka yalithibitishwa.

Kutokana na maelezo hayo, majaji hao walisema hawaoni sababu ya kuiona hukumu ya mwanzo ya adhabu ya kifo kama ina makosa yoyote kama ushahidi uliowatia hatiani ulivyochambuliwa, hivyo adhabu ya kifo inabaki pale pale.

Kutokana na uamuzi huo wa mahakama ya juu kabisa kwa Katiba ya Tanzania, wauaji hao wamefika mwisho katika kupambana kupangua adhabu hiyo ya kunyongwa hadi kufa, isipokuwa labda wapate msamaha wa Rais.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live