Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kitanzi chamng’ang’ania aliyeua walinzi wawili wa Kimasai

Hukumu Pc Data Kitanzi chamng’ang’ania aliyeua walinzi wawili wa Kimasai

Wed, 21 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, limebariki adhabu ya kifo aliyopewa mmoja wa mafundi waliokuwa wanajenga kituo cha kuuza mafuta Jijini Dodoma, Menroof Haule aliyewaua walinzi wawili wa kimasai.

Hukumu ya kubariki adhabu hiyo imetolewa Februari 20, 2024 na majaji Augustine Mwarija, Rehema Kerefu na Mustafa Ismail, ambao wamesema kuwa kesi ya upande wa Jamhuri ilikuwa imethibitishwa pasipo kuacha mashaka.

Hivyo majaji hao wamezitupa sababu 12 alizokuwa ameziwasilisha mbele ya Mahakama ya Rufani akijaribu kujinasua na adhabu ya kifo aliyokuwa amehukumiwa Aprili 11, 2022 na Jaji Adam Mambiwa Mahakama Kuu kanda ya Dodoma.

Maelezo yake mwenyewe ya kukiri kosa akisimulia hatua kwa hatua namna alivyowaua walinzi hao kwa kuwaponda vichwa kwa kutumia sululu, ndio yalimmaliza ambapo majaji wamesema ushahidi dhidi yake ulikuwa mzito.

Walinzi hao wawili, Paulo Nduluma na Aloyce Patsango, waliuawa Agosti 4,2015 na maiti zao ziligunduliwa saa 11:00 alfajiri na mama lishe, Bilha Yaho ambaye ana kawaida ya kuwauzia chakula mafundi waliokuwa wanajenga kituo hicho.

Kama ulivyo utaratibu wake, siku hiyo alifika eneo la ujenzi na kuanza kuwaita walinzi hao bila mafanikio, ambapo aliamua kuingia ndani kuchota maji ili kusafisha vyombo, ndipo alipoona damu ukutani na baadaye miili ya walinzi hao.

Baada ya kuona hivyo, aliwapigia simu mafundi wengine ambao nao walimjulisha msimamizi wa ujenzi huo na taarifa zikafikishwa Polisi, ambao walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi na baadaye kumkamata Haule Agosti 9,2015.

Mashahidi sita wa Jamhuri wakiwemo askari wawili waliochunguza mauaji hayo, walisema katika uchunguzi wao walibaini kasha (container), lililokuwa linahifadhi mifuko ya saruji likiwa limevunjwa na mifuko 60 ilikuwa imeibwa.

Kulingana na ushahidi huo, Haule alipokamatwa na Polisi, alikiri kufanya mauaji hayo na kuiba mifuko hiyo 60, ambapo maelezo yake ya onyo yaliandikwa na baadaye akapelekwa kwa mlinzi wa amani na kuandika maelezo ya ungamo.

Maelezo ya ungamo

Sehemu ya maelezo yake ya onyo aliyoyaandika Polisi, muuaji huyo anaeleza “Ilipofika tarehe 4.8.2015 nikaingia kazini asubuhi nikafanya kazi nikamaliza saa 11 jioni na kuacha Sululu ndani ya shimo lenye futi tano,”

Anaendelea kueleza “Majira ya saa 2:00 usiku nikiwa tayari nimekwishapitia pale shimoni na kuchukua sululu tayari kwa kuwavizia walinzi wa kimasai na kuwaua kabisa, walikaa wakiwa wanaongea kwa muda hadi saa 6:00 usiku”

“Ndipo nikawaona wametawanyika na kila mmoja ameelekea kulala. Mmoja akapanda kwa juu na mwingine akalala kwa chini. Nikakaa kidogo kuwasubiria usingizi uwapitie kwanza kwa muda wa nusu saa hivi.”

“Ndipo nikaona muda ule unatosha nikavua viatu vyangu na kuviacha nje kwenye banda la mama lishe nikarudi nikaruka ukuta nikatembea kwa kuambaa ambaa na ukuta huku nikinyata hadi sehemu ya juu ya jengo nikamkuta Mmasai amelala,”

“Nikiwa nimeshikilia sululu mkononi ambayo ilikuwa imekatika upande mmoja, nikampiga na sululu kichwani mara mbili kwa kutumia upande ule uliokatika nikahakikisha hatikisiki kabisa. Nikashuka kumtafuta mmasai mwingine.”

“Nikamkuta na yeye amelala nikampiga kichwani mara tatu kwa kutumia ile sululu na kumpasua kichwa naye hakuamka wala kutikisika. Ndipo nikapata wazo la kwenda kuvunja kontena (kasha) ili nichukue cement (saruji).

Sehemu ya maelezo yake aliyoyaandika kwa mlinzi wa amani ambaye ni Hakimu, alieleza “Kuanzia saa 2 usiku nilianza kuwavizia kujua wanalala wapi. Nilipoona wamelala usiku huo, niliamua kuwafuata na kuwapiga na kitu kizito kichwani”

“Nikawaona wote wamekufa baada ya kuwagonga, walikuwa wawili. Nilipojua wamekufa nilichukua nyundo nikafungua kontena nikachukua mifuko ya cement (saruji) jumla mifuko 60…”, ameeleza muuaji huyo katika maelezo yake ya ungamo.

Alivyojitetea ili kujinasua lakini wapi

Katika utetezi wake, muuaji huyo anayesubiri kunyongwa kama Rais ataweka saini yake, alikiri kuwa mmoja wa mafundi katika eneo la ujenzi na anawafahamu marehemu, walikuwa ni marafiki wakubwa na hawakuwahi kugombana.

Akaeleza kuwa mchana wa Agosti 3,2015, alikwenda katika eneo la ujenzi na kukaa na marehemu (walinzi) kwa amani kabisa na Agosti 4,2015 ndipo akajulishwa kuwa na shahidi wa kwanza (mama lishe) kuwa wameuawa.

Pia akakiri kuwa Agosti 9, 2015 alikamatwa akihusishwa na mauaji hayo na akadai kuwa aliteswa alipokamatwa lakini hata hivyo akakiri kuandika maelezo hayo ya onyo na ya ungamo, ambayo tayari yalikuwa yamepokelewa kama kielelezo.

Pamoja na utetezi huo, Jaji alimtia hatiani kwa kuzingatia mazingira ya tukio na maelezo yake mwenyewe ya kukiri kufanya mauaji hayo, ambayo Jaji alisema yalieleza kila kitu namna alivyoua hivyo akamuhukumu adhabu ya kifo.

Hakuridhika na adhabu hiyo ya Jaji Dk Adam Mambi ndipo akakata rufaa Mahakama ya Rufani ambayo hata hivyo ilibariki maamuzi ya Mahakama Kuu iliyomuhukumu kunyongwa hadi kufa, wakisema rufaa yake haina mashiko.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live