Moshi. Agosti 7, 2013 Jiji la Arusha na miji ya Moshi na Mirerani ilitikiswa na taarifa za kuuawa kwa kupigwa risasi, mfanyabiashara maarufu wa madini, Erasto Msuya maarufu kama Bilionea Msuya, tukio lililotokea katika Wilaya ya Hai.
Katika tukio hilo, wauaji waliokuwa na pikipiki walitumia mbinu ya kumshawishi kumuuzia madini ya Tanzanite na kumvuta hadi eneo la Orkolili Mijorohoni, ambapo walimminia risasi 22 kwa kutumia bunduki aina ya Submachine Gun (SMG).
Mwili wake ulikutwa na matundu 26 ya risasi, madogo 13 yakiwa ni sehemu ambayo risasi ziliingia na 13 ya risasi zilipotokea. Risasi hizo zilichakaza utumbo mwembamba, kuharibu figo, mishipa ya damu na bandama.
Je, unafahamu kuwa watu wawili waliokwenda kufanya mauaji walikodiwa kwa dau la Sh5 milioni kila mmoja na wawili waliopewa kazi ya kuwalinda wauaji ili watekeleze mpango huyo walilipwa Sh3 milioni kila mmoja?
Je, unafahamu kuwa bunduki iliyotumika katika mauaji hayo ilinunuliwa Namanga, Kenya kwa Sh4 milioni? Katika mfululizo wa makala haya tunakuletea simulizi ya mauaji hayo tukiegemea ushahidi ulitolewa na wa mashahidi 27 wa Jamhuri katika kesi ya mauaji hayo.
Katika kesi hiyo iliyosikilizwa na Jaji Salma Maghimbi, mashahidi 27 waliotoa ushahidi wa moja kwa moja, watano ushahidi wao ulisomwa na vielelezo vilivyowasilishwa ni 27.
Kesi hiyo ilipoanza, washtakiwa walikuwa saba, Sharifu Mohamed, Shahibu Jumanne, Mussa Mangu, Jalila Zuberi, Karim Kihundwa, Sadick Jabiri na Ally Majeshi.
Hata hivyo, mmoja wao, Jalila Zuberi aliachiwa Mei 14, 2018 baada ya kuonekana hana kesi ya kujibu.
Hadi kesi hiyo inafika mwisho na Jaji Maghimbi kutoa hukumu Julai 23, 2018, washitakiwa watano walitiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu ya kifo na mshtakiwa wa pili, Shahibu Jumanne maarufu “Mredii” aliachiwa huru.
Washtakiwa katika kesi hiyo walitetewa na jopo la mawakili wanne, Harrison Ndusyepo, Majura Magafu, Emmanuel Safari na John Lundu huku jopo la upande wa Jamhuri ukiongozwa na Neema Mwanda, wakili mwandamizi wa Serikali mkuu.
Baada ya kutiwa hatiahia washtakiwa hao walikata rufaa, na aliyefanikiwa kuchomoka ni mrufani wa pili pekee, Mussa Juma Mangu ambaye jopo la majaji wa Mahakama ya Rufani iliyoketi Dar es Salaam kubaini kuwa ushahidi dhidi yake haukuthibitisha kosa.
Shahidi wa kwanza
Shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri alikuwa Mrakibu wa Polisi (SP) Joash Yohana, aliyekuwa mkuu wa upelelezi (OC-CID) Wilaya ya Hai, aliyeeleza kuwa Agosti 7, 2013, alipokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) akimjulisha juu ya mauaji ya Msuya.
Bosi wake huyo alimjulisha kwa simu kuwa alikuwa amepokea simu kutoa kwa raia wema kuwa kuna mfanyabiashara wa madini kutoka Mirerani ameuawa kwa kupigwa risasi, katika eneo la Orkalili karibu na eneo la KIA.
“Baada ya kupokea hiyo taarifa niliondoka na wasaidizi wangu kwa haraka kuelekea eneo la tukio na tulipofika tulikuta mwili wa marehemu amelala kwa tumbo na ulikuwa na matundu mengi ya risasi,” alieleza shahidi.
“Mwili wake ulikuwa unavuja damu nyingi. Tulipompekua pamoja na kupekua gari tulimkuta na silaha aina ya bastola ikiwa na magazine mbili. Ile ndogo ilikuwa na risasi sita na ile magazine kubwa ilikuwa na risasi 23,” alisema SP Yohana.
“Katika mwili wake tulimkuta na simu mbili moja Samsung nyeusi na Iphone. Tulipoona mwili wake ulikuwa na matundu mengi ya risasi kifuani, tuliamua kuchunguza eneo lile na tulifanikiwa kupata maganda 22 ya bunduki ya SMG”.
“Gari la marehemu Range Rover namba T 800 CKF lilikuwepo na halikuonyesha kuharibika kwa lolote na hii iliashiria kuwa marehemu alitoka mwenyewe kwenye gari kwa hiyari,” alieleza na kuwa baadaye aliondoka kwenda eneo lingine.
Huko kwenye eneo lingine ambalo ni umbali wa kilometa nane, walikuta kofia ngumu (helmet) ya rangi ya fedha, pikipiki yenye namba T316 CLV na jaketi la rangi ya kaki, ambavyo walielezwa vilitelekezwa na waliofanya mauaji ya Msuya.
Baada ya hapo, mkuu wa upelelezi wa Mkoa Kilimanjaro (RCO), Ramadhan Ng’anzi alifika na timu yake ya masuala ya uhalifu wakiwemo wapiga picha, wataalamu wa alama za vidole na baadaye alikabidhi vielelezo vyote alivyokusanya kwa timu hiyo.
SP Yohana akiongozwa na Wakili Chavula kutoa ushahidi wake, aliomba kutoa simu mbili za marehemu zipokewe kama kielelezo, lakini mawakili wa utetezi walipinga kwamba shahidi hakuwa amevitambua vizuri, mahakama ilikubali pingamizi.
Shahidi huyo aliendelea kueleza kuwa katika eneo mauaji yalipotokea, waliokota maganda 22 ya risasi za SMG ambayo aliyatambua mahakamani na kueleza kuwa pia walikuta bastola aina ya Gesel ikiwa na magazine 2 na jumla ya risasi 30.
Katika kuhitimisha ushahidi wake, shahidi huyo aliyatambua maganda ya risasi za SMG aliyoyakuta eneo la tukio na akaiomba mahakama ihamie eneo la maegesho ili iweze kulitambua gari la marehemu walilolikuta eneo la tukio.
Akijibu swali la Wakili Ndusyepo kama maganda hayo ya risasi hayawezi kuwa yalifyatuliwa kutoka bunduki aina ya SAR au AK47, shahidi huyo alisema kwa uzoefu wake wa miaka 21 ya upelelezi, risasi hizo zilifyatuliwa na SMG.
Dodoso za mawakili
Kwa upande wa Wakili Magafu alimtaka shahidi huyo aeleze kama bunduki alizozitaja AK47, SMG na SAR kama zinatumia risasi zinazofanana, alisema hazitumii risasi zinazofanana na kuwa polisi hutumia silaha hizo kwa malengo tofauti tofauti.
Akijibu swali la Wakili Safari aliyetaka aieleze mahakama ni eneo gani hasa waliona majeraha ya risasi, alisema majeraha yalikuwa katika maeneo mengi na hawezi kukumbuka hasa ni maeneo yapi na kwamba mwili ulikuwa na matobo mengi.
Shahidi huyo katika maswali hayo ya dodoso, alisema katika uchunguzi wake, pikipiki ilitelekezwa na wahalifu waliofanya mauaji hayo wakati wakitoroka.
Akijibu maswali ya dodoso kutoka kwa Wakili Lundu, shahidi huyo alisema kwa kawaida maganda ya risasi hupatikana uelekeo ilipofyatuliwa na kwa maeneo walipoyakuta, inaonyesha risasi zote 22 zilifyatuliwa kuelekea kwa marehemu.
“Tulijulishwa na watoa taarifa mahali wahalifu walipotorokea kwa pikipiki na hili walitueleza watu wengi. Hatukuwauliza kwa nini hawakuzuia uhalifu huo usitendeke. Hatukuwa na muda wa kuuliza lakini ushahidi umebaini nani walifanya,” alisema.
Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, upande wa utetezi uliibua hoja kuwa mtu aitwaye Shujaa Baruti ni shahidi wa upande wa mashtaka na alikuwepo wakati kesi inaendelea, lakini upande wa mashitaka ukasema ni sehemu ya mashahidi.
Usikose kusoma mwendelezo wa kesi hii kesho