Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kina Kalugendo waomba DPP kuiondoa kesi inayowakabili

84499 Utetezi+pic Kina Kalugendo waomba DPP kuiondoa kesi inayowakabili

Sat, 16 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upande wa utetezi  katika kesi inayowakabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Uthaminishaji Almasi na Vito Tanzania (Tansort), Archard Kalugendo na mwenzake umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam kuwa kama hawana nia ya kuendelea na shauri hilo waliondoe mahakamani hapo.

Mbali na Kalugendo mwingine aliyekuwa Mthamini wa Madini ya Almasi wa Serikali, Edward Rweyemamu wanakabiliwa na  kesi ya uhujumu uchumi namba 54/2017, kwa kuisababishia Serikali ya Tanzania hasara ya Sh2.4 bilioni.

Wakili wa utetezi, Francis Makota alidai hayo leo Ijumaa Novemba 15, 2019 baada ya wakili wa Serikali, Grory Mwenda kudai jalada la shauri hilo lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP) na upelelezi bado haujakamilika.

Makota alidai upande wa mashtaka wamekuwa wakisema  jalada lipo kwa DPP hivyo kama hawana nia watafute njia nyingine ya kuliondoa mahakamani hapo.

"Tunawaomba upande wa mashtaka  waongeze kasi kwa kuwa washtakiwa wapo ndani kwa muda mrefu kama hawana nia ya kuendelea na shauri hili watafute njia nyingine ya kuliondoa," alidai Makota.

Naye Wakili wa Utetezi, Nehemia Nkoko alidai kuwa  kama kuna uwezekano mahakama hiyo iwaruhusu kuonana  na DPP ili kufuatilia hilo jalada.

Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi aliwataka upande wa mashtaka kufuatilia jalada kwa DPP na shauri hilo limeahirishwa hadi Novemba 29, 2019 kwa ajili ya kutajwa.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Agosti 25 na 31, 2017 katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga.

Kwa pamoja na kwa vitendo vyao wakiwa wathaminishaji wa Almasi wa Serikali na waajiriwa wa wizara ya nishati na madini, waliisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 1,118,291.43 ambazo ni sawa na Sh2.4 bilioni.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz