Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kimiti atoboa siri za ATCL

31452 Atcl+pic AIR Tanzania

Thu, 13 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Paul Kimiti (73) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa aliamua kujiuzulu wadhifa wake wa ujumbe wa bodi katika Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) baada ya kubaini kuwa menejimenti ya shirika hilo ilikuwa inakodi ndege bila kufuata utaratibu.

Alidai menejimenti ya ATCL ilifanya uamuzi mbaya wa kukodi ndege bila kuishirikisha bodi, jambo lililosababisha hasara kwa Serikali.

Kimiti ambaye alishawahi kuwa mbunge wa Sumbawanga (CCM), aliieleza mahakama hiyo jana, wakati akitoa ushahidi wake katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh71 bilioni, inayomkabili aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa ATCL, David Mattaka na wenzake wawili.

Akiongozwa na wakili wa Serikali Mwandamizi, Vitalis Peter mbele ya Hakimu Augustino Rwenzile, Kimiti alidai aliteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya ATCL mwaka 2007 hadi 2009 alipojiuzulu.

Alidai kuwa menejimenti ya ATCL ilikodi ndege aina ya Airbus 320-214 kutoka kampuni ya Wallis Treding, bila kuishirikisha bodi.

Kimiti alidai kipindi chote alichokuwa mjumbe wa bodi hiyo, hawajawahi kushirikishwa katika uamuzi wa kukodi ndege, hivyo menejimenti ilikuwa imefanya makosa kwa mujibu wa sheria.

Alidai kuwa baada ya wizara kukaa kimya bila majibu kuhusiana na suala hilo aliamua kujiuzulu.

Alibainisha kuwa moja ya majukumu yake kama mjumbe wa bodi ni kutoa ushauri kwa menejimenti, kutoa ushauri wa utekelezaji wa majukumu ya shirika na kuidhinisha utekelezaji wa jambo lolote ambalo ATCL inataka kutekeleza.

Baada ya shahidi huyo kumaliza kutoa ushahidi, hakimu Rwenzile aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 21, 2019 itakapoendelea.

Mbali na Mattaka, washtakiwa wengine ni vigogo kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ambao ni ofisa mtendaji mkuu mstaafu, Dk Ramadhan Mlinga na mwanasheria Bertha Soka.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Oktoba 9, 2007, Mattaka anadaiwa kusaini mkataba kwa ajili ya kukodisha ndege na Andrew Wettern kwa niaba ya kampuni ya Wallis Trading Inc na kwamba mkataba huyo unadaiwa kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh 71bilioni.



Chanzo: mwananchi.co.tz