Moshi. Jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro kwa kushirikiana na kikosi maalum cha kuzuia Magendo cha Mamlaka ya mapato nchini (TRA) wamekamata zaidi ya kilogramu 700 za mirungi zinazodhaniwa kutokea nchi jirani ya Kenya.
Akizungumza jana Agosti 7 na waandishi wa Habari mkoani hapa Kamanda wa Jeshi la Polisi Kilmanjaro, Hamis Issah amesema gari hilo lilionekana asubuhi katika barabara ya Arusha-Moshi.
Amesema kikosi maalum cha polisi kwa kushirikiana na TRA walilitilia shaka gari ambalo lilionekana limebeba mzigo mkubwa na kulifuatilia.
“Baadaye gari hilo baadaye lilitelekezwa karibu na daraja la Karanga mjini Moshi,” amesema.
Kamanda Issah amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa gari hilo ni la nchi jirani ya Kenya.
Kamanda Issa alisema kuwa wanamtafuta mmiliki wa gari hilo ili kujua ni nani aliyehusika na usafirishaji huo wa mirungi ili kuchukua hatua kali za kisheria na kumpeleka kwenye vyombo husika.
“Tunawaambia wananchi kuwa tumejipanga na matukio kama haya tunahakikisha wale wote waliojihusisha na biashara hii tunawakamata na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria kwani tukio hili ni la jinai,”amesema Kamanda Issah.
Kwa upande wake, Meneja wa TRA,Mkoa wa Kilimanjaro Msafiri Mbibo amesema kikosi chao maalum cha kuzuia magendo (fast team) kililitilia shaka gari hilo ndipo wakalifuatilia ili kujua limebeba mzigo gani lakini baada ya mhusika kujua gari hilo linafuatiliwa alikimbia.
“Tulilikamata gari hilo likiwa na mzigo mkubwa wa mirungi na tulipima uzito wa mirungi hiyo tukapata una zaidi ya kilo 700 pamoja na vitu vingine ambavyo vilikua kwenye gari,ni pamoja na vitambulisho vyenye usajili wa gari hilo,funguo ambavyo vitatusaidia kumpata mhusika kirahisi,”amesema Mbibo.