Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilio kingine kwa askari polisi

Kilio Tena Polisi Kilio kingine kwa askari polisi

Tue, 15 Mar 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Kila linapotajwa jina la Jeshi la Polisi, Santus Galus Yondani (41) anapatwa na hisia zinazomkumbusha uchungu wa jinsi alivyokamatwa, kuteswa na kuporwa mali.

Anadi matukio hayo alifanyiwa na askari polisi waliomhusisha yeye na wenzake na wizi wa Sh159 milioni, mali ya mfanyabiashara maarufu wa jijini Dodoma.

“Wamenikamata bila kosa na kunifanya niishi mahabusu siku 563. Wameishia kunipora mali zangu zote, wamechukua mifuko 443 ya simenti na pikipiki zangu, wamechukua gari langu na Sh6.3 milioni, simu zangu na kadi za benki. Hawataki kunirudishia,” anasema Yondani kwa uchungu.

Hivi sasa Yondani yuko huru baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka kupeleka taarifa Mahakama ya Wilaya ya Singida kuwa hana tena nia ya kuendelea na kesi dhidi yake na wenzake iliyofunguliwa Agosti 28, 2020.

Hata hivyo, kijana huyo ambaye alianza kuwa na mafanikio kibiashara anashindwa kufurahia uhuru alioupata akidai kupoteza mali nyingi mikononi mwa askari na kuachwa maskini.

Anadai polisi hawataki kumrudishia mifuko 443 ya simenti, pesa taslimu Sh5.3 milioni, kadi za benki na pesa Sh1 milioni waliyoitoa kutoka kwenye simu yake ya mkononi baada ya kuteswa.

Anamtaja askari polisi mmoja (jina tunalo) kuwa ndiye aliyemtesa na kumlazimisha atoe namba ya siri ya benki na kutoa pesa kwenye simu yake.

Maelezo ya Yondani na wenzake yanatoa wito si tu kwa mamlaka za utoaji haki kuchunguza madai yake na wenzake bali pia kwa polisi kuwachunguza askari wanaotuhumiwa.

Ilivyokuwa

Ilikuwa mchana wa Agosti 10, 2020 siku Yondani alipoanza safari akitokea Kibaha, Mkoa wa Pwani, kwenda Kilombero, Morogoro akiwa na watoto wake wawili (Stanley na Greyson).

Bila kujua kuwa safari hiyo ilikuwa mwanzo wa safari mpya ya kukamatwa, kuteswa na kunyang’anywa mali, kijana huyo aliendesha gari lake aina ya Toyota Noah hadi Chalinze ambapo alisimama ili anunue matunda.

“Nilipotaka kufungua mlango ghafla nikaonyeshewa bastola na askari, wote wa Dodoma, wakaniambia nishuke na moja kwa moja wakanipakia kwenye Toyota Prado nyeupe. Watoto wangu pia wakapakiwa,” anaeleza.

Anasema ndani ya Prado alikuwepo askari mwingine na dereva aliyekuja kujulikana kama mfanyakazi wa mfanyabiashara wa vinywaji vikali Dodoma, Alex Edmund Lupindo, aliyekuwa akilalamika kuibiwa Sh159 milioni.

Uporaji mali

Mwananchi limebaini kuwa wawili kati ya askari watatu waliomkamata Yondani na kudaiwa kupora mali zake ni miongoni mwa watu tisa waliokamatwa Desemba mwaka juzi jijini Arusha kwa kumteka na kumwomba rushwa ya Sh30 milioni Mwenyekiti wa Chama cha Wauzaji Madini Tanzania (Tamida), Sammy Mollel.

Askari Gasper Paul na Bryton Murumbe wanadaiwa kushiriki kumteka Mollel anayemiliki kampuni ya Germs na Rock Ventures baada ya kujitambulisha kuwa wao ni askari kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Dodoma kikosi maalumu kinachofuatilia ukwepaji kodi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Onesmo Lyanga amesema hahusiki na askari hao wanaodaiwa kutoka Makao Makuu ya Polisi, Dodoma. “Kama ni wa makao makuu hao sio wangu, mimi huko siko,” alisema.

Polisi Chalinze

Baada ya kukamatwa Yondani alipelekwa hadi Kituo cha Polisi Chalinze. Akiwa kituoni, polisi walitaka awaeleze kama anamfahamu mtu aitwaye Yohana.

Yohana Edmund Lupindo ni mdogo wa mfanyabiashara wa Dodoma Alex Edmund Lupindo anayedaiwa kuripoti kuibiwa Sh159 milioni na mdogo wake huyo na washirika wake katika duka lake la vinywaji mkoani Singida, lililo chini ya kampuni ya Takawedo Investment Limited.

Baada ya kukana kumjua Yohana, askari walichukua simu yake na kuanza kuchunguza mawasiliano yake kwa lengo la kujua kama aliwahi kuwasiliana naye.

Yondani anasema baada kukana alipelekwa ‘gereji’ ambako ni chumba kilichokuwa na meza mbili. “Wakanifunga pingu, wakachukua miguu wakaiingiza katikati ya mikono, wakapitisha nondo kati ya miguu na kunining’iniza kati ya zile meza mbili kwa staili waliyokuwa wakiita popo.

“Pale wakanipiga sana, wakataka niseme kama namfahamu Yohana Edmund Lupango. Nikasisitiza simjui mtu huyo. Wakanitoa ‘gereji’ nikiwa na maumivu makali na safari ya kuja Dar es Salaam ikaanza alisema.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Pius Lutumo ameliambia Mwananchi kuwa hajawahi kupata taarifa za kijana huyo kuteswa Chalinze.

“Tangu Agosti 2020 uongozi umebadilika sana. Naomba tu afuate procedure (utaratibu) wa kulalamika. Kama aliwahi kulalamika na hajasaidiwa mnaweza kumwelekeza akaja kwangu,” alisema.

Akiendelea kuelezea Yondani alisema “Zamu hii tulielekea Mbagala Kongowe kwa mtu aitwaye Mohamed Hamidu Mohamed (80) na tukawasili pale saa nne usiku. Tulimkuta, polisi walimchukua na kumuingiza ndani ya Prado na kuanza kumpiga. Walitaka naye aeleze anamfahamu vipi Yohana,” anasimulia.

Kwa mujibu wa Yondani, usiku huo walipelekwa Kituo cha Polisi Ufundi, Kurasini na siku iliyofuata walihamishiwa Kituo cha Polisi, Oysterbay walipoendelea kuteswa huku wakitakiwa watoe fedha ili waachiwe” anasema.

“Kwanza sikuwa na Sh10 milioni walizoniomba. Kwenye gari nilikuwa na Sh5.3 milioni, kadi za benki na za kwenye simu walizichukua wao,” anasema.

Wakati anakamatwa, tayari Yondani alikuwa na mafanikio katika bishara zake. Alikuwa akimiliki duka kubwa la simenti na baa huko Kilombero. Pia, alikuwa na pikipiki nyingi za kukodisha na wakati mwingine alijihusisha ya ununuzi na uuzaji wa madini.

Anadai jioni ya Agosti 11, 2020 akiwa bado mikononi mwa polisi, askari waliomkamata walianza tena kumpiga miguu na mikono kipigo walichokiita popo.

“Mwisho nikalazimishwa nitaje namba yangu ya siri ya benki. Kipigo kilipozidi nikawapa, wakaenda kutoa Sh1 milioni kutoka akaunti yangu ya NMB na kuzituma kwenye namba yangu ya tigo 0717 742961 halafu wakazituma tena kwenye namba wanayoijua na kuzitoa. Walifanya hivyo ionekane kuwa mimi ndiye niliyetoa zile pesa kwa hiari yangu.

Safari ya Kilombero

Siku iliyofuata, Agosti 12, 2020 saa nane mchana Yondani na Mohamed walitolewa mahabusu na kuanza safari ya kuelekea Kilombero. Saa tatu usiku waliingia Kituo cha Polisi Ruhembe.

“Ruhembe wakakataa tusilale, wakatupeleka kituo cha K1 lakini Mkuu wa Kituo akakataa, wakatupeleka Kituo cha Polisi Nyandeo, pale tukalala siku moja,” anasema Yondani.

Siku iliyofuata polisi waliongozana nao na kuanza shughuli ya upekuzi.

“Baada ya kuchukua wakaenda kuvunja duka langu la simenti bila hata kuwa na hati ya kukamata mali wala kuwataarifu viongozi wa Serikali ya Mtaa. Wakamnyang’anya funguo mfanyakazi wangu,” anasema.

Anadai baada ya zoezi hilo walirudishwa tena Kituo cha Polisi cha K1 na kulala huko. Siku iliyofuata Agosti 15 walitolewa na kupelekwa kituo cha K2.

“Pale nilishangaa nikakuta pikipiki yangu ya miguu mitatu na pikipiki zangu nyingine zimepaki pale kituoni. Nikabaki nashangaa zimekujaje pale,” anadai.

Wakati huo wote, watuhumiwa hao na askari walikuwa wakitumia gari aina ya Toyota Prado wanalodaiwa kupewa na mfanyabiashara aliyedai kuibiwa ili wamfanyie kazi yake.

Mwananchi liliwasiliana na mmiliki wa Takawedo, Alex Lupindo ambaye hakukubali wala kukanusha madai kuwa aliwapa polisi gari lake litumike kuwasaka na kuwakamata watuhumiwa

Kuchukua mali

Agosti 15, 2020 asubuhi alidai polisi walimtoa mahabusu na kuongozana naye tena hadi dukani kwake wakifuatana na magari mawili aina ya Isuzu Fusso.

“Kwa kuwa walikuwa na ufunguo wa duka walifungua mlango wakaanza kupakia simenti yangu kwenye Fusso. Wakati huo mpiga picha wao aliyeitwa Steven Milele alikuwa akipiga picha. Tulikuwa pamoja na OC-CID wa Ruhembe anaitwa Rasio.

“Wakabeba mali zote. Walipomaliza magari yote yakaelekea hadi kituoni na kule wakapakia pikipiki zangu na safari ya kuelekea Morogoro ikaanza na walifikia kwenye hoteli moja na kukutanishwa na Alex Lupindo, tajiri aliyedai kuibiwa.

“Tulipofika wakamwambia ‘hawa hapa bosi tumewaleta’. Yeye akajibu palepale ‘mimi sitaki kesi nataka mali zenu,’” anasema Yondani. “Akasema kama hatutaki kuachia mali tupelekwe kituoni au kama tuko radhi amwite mwanasheria tuandikishane tumalize kesi.

Hata hivyo, Lupindo amekana kukutanishwa hotelini na watuhumiwa hao. “Sijawahi kukutana nao wala sidhani kama kesi yao imefutwa,” alisema.

Yondani anadai baada ya mazungumzo na Lupindo kutozaa matunda walirudishwa Kituo Kikuu cha Polisi Morogoro na kulala pale kwa siku tatu tangu Agosti 15, 2020.

Msafara kuelekea Singida

Agosti 18 msafara ulianza kutoka Morogoro hadi Kituo Kikuu cha Polisi Dodoma ambapo walilala na siku iliyofuata walielekea Singida.

Wakiwa Singida, Yondani na mwenzake Mohamed walikaa mahabusu kwa siku 9 na Agosti 28, 2020 Yondani, Mohamed walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Singida na kushtakiwa kisha kuwekwa ndani bila dhamana.

Waachiwa

Februari 28, 2022 ikawa siku ya bahati kwao. Mahakama ya Wilaya ya Singida iliwaachia huru baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka kupeleka taarifa ya kutokuwa na nia ya kuendelea kesi hiyo.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz