Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilichotokea mahakamani kesi ya 'Papa Msofe'

91714 Pic+musofe Kilichotokea mahakamani kesi ya 'Papa Msofe'

Tue, 14 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam . Upelelezi wa kesi ya kutakatisha fedha, inayomkabili mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Marijan Msofe (53) maarufu kama 'Papa Msofe' na wenzake watano, haujakamilika.

Msofe na wenzake wanakikabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kujipatia Sh943 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladslaus Komanya akisaidiana na Sylvia Mitanto ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam leo Jumatatu Januari 13, 2020 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Komanya ameeleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo anaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Isaya baada kusikiliza maelezo hayo ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 27, 2020 itakapotajwa.

Mbali na Msofe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 124/2019 ni wakili wa kujitegemea Mwesigwa Mhingo(36), Wenceslau Mtui(49), Fadhil Mganga(61), Josephine Haule(38) na Emmanuel  Reuben (32).

Miongoni mwa mashtaka yao ni kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, ambapo washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo, kati ya Desemba 2018 na Septemba 2019, Jiji la Dar es Salaam.

Inadaiwa kuwa wakiwa na nia hiyo walijipatia dola za Kimarekani 300,000 (Sawa na Sh.660milioni) kutoka kwa Pascal Camille, wakidai kuwa watamuuzia dhahabu kilo 200 ambayo wangemsafirishia kwenda Ureno wakati wakijua si kweli.

Pia wanadaiwa katika kipindi hicho,  walimlaghai Johnson Mason kwamba watamuuzia kilo 20 za dhahabu yenye thamani ya Sh253 milioni na wangemsafirishia kwenda nchini Ureno wakati wakijua si kweli.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka kutakatisha fedha linawakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa Kisutu, Desemba 2, 2019 wakikabiliwa na mashtaka hayo.

Chanzo: mwananchi.co.tz