Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili fanyabiashara Jiteshi Ladwa, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirishwa mpaka Julai 18 mwaka huu itakapotajwa tena kwa ajili ya taratibu nyingine kutokana na Hakimu kuwa likizo fupi.
Jitesh anakabiliwa na mashtaka ya kujipatia pesa kwa njia za udanganyifu na utakatishaji fedha, akidaiwa kujipatia jumla ya Sh601,849, 736 (zaidi ya Sh601.84 milioni kutoka kwa wapangaji wa nyumba za kampuni ya Msasani Peninsula Flats Ltd.
Anadaiwa kutenda kosa hilo baada kughushi barua kuonesha kuwa kampuni ya Msasani Peninsula Ftats imeiteua kampuni ya Indian Ocean, kuwa wakala mkuu wa mali zake kwa ajili ya kukusanya kodi kutoka kwa wapangaji.
Kesi hiyo imetajwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mfawidhi, Godfrey Isaya, kwa niaba ya Hakimu Mkazi Mkuu, Evodia Kyaruzi anayesikiliza kesi hiyo katika hatua ya awali kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu, kwa kuwa yuko likizo fupi.
Hata hivyo Jitesh anayewakilishwa na jopo la mawakili linaloongozwa na Jeremiah Mtobesya, limewasilisha pingamizi la kisheria kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo. Mshtakiwa amerudishwa mahabusu kutokana na kukabiliwa na shtaka la utakatishaji fedha lisilo na dhamana.
Jitesh ni mmoja wa wanahisa wa kampuni hizo za Msasani Peninsula na Indian Ocean Hotels Limited inayomiliki hoteli za Golden Tulip, Masaki; ambazo zinamilikiwa kwa ubia na wanafamilia wa familia ya aliyekuwa mfanyabiashra maarufu Walji Ladwa.
Anadaiwa kuwa akiwa mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Indian Ocean Hotels Limited, alitumia fursa hiyo kuonesha kuwa anastahili kuopata pesa hizo zilizokusanywa kwa wapangaji mbalimbali.
Katika kesi hiyo, Jiteshi anakabiliwa na jumla ya mashtaka manane ya kughushi nyaraka, kujipatia pesa kwa njia za udanganyifu na utakatishaji fedha, akidai kutenda makosa hatyo kwa nyakati tofauti kati ya Septemba 2019 na Aprili 2022.