Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kikongwe auawa, anyofolewa sehemu za siri

35664 Kikongwepic Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi

Thu, 10 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bukoba. Polisi mkoani Kagera wameanza msako wa kuwabaini waliohusika na mauaji ya Laurian Kakoto (80), ambao walimnyofoa korodani na kuzika nusu ya mwili wake uliokutwa ukiwa na majeraha ya kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni.

Akizungumza jana mjini Bukoba, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi alisema tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Ihunga, Kata ya Kishanda, Muleba Jumatatu iliyopita.

Alisema kabla ya tukio hilo, marehemu aliaga nyumbani kwake kuwa anakwenda kununua unga na mchele dukani.

Alisema sehemu ya mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa umefukiwa ardhini katika shamba la mahindi huku mfuko wa mchele ukiwa pembeni.

Kamanda huyo alisema baada ya mwili huo kufukuliwa ilibainika kuwa baadhi ya viungo vimeondolewa, “na katika hilo shimo walilochimba kumfukia walianza kuingiza kichwa na miguu kubaki juu,” alisema, “Wananchi waliokuwa wakipita jirani na ulipofukiwa mwili huo walibaini tukio hilo.”

Katika tukio jingine, Kamanda Malimi alisema dereva bodaboda, Albert Antipas aliuawa katika Kijiji cha Kibingo wilayani Kyerwa, tukio lililosababisha nyumba 16 kuteketezwa kwa moto na wananchi kwa madai ya kulipiza kisasi.

Alisema Antipas alikutwa ameuawa baada ya kuporwa pikipiki Januari 2 na mwili wake kupatikana Jumatatu iliyopita ukiwa umefungwa mikono pamoja na jiwe na kutupwa katika bwawa la kufugia samaki.

“Zaidi ya watu 300 walihamasishana wakiwa na silaha za jadi kwenda kuchoma nyumba 16 na kukata migomba na kahawa thamani yake bado haijajulikana. Chanzo ni kuwatuhumu kuhusika na mauaji dereva huyo,” alisema.

Alisema watu wasiojulikana walimkodisha dereva huyo wakitaka awapeleke eneo la Murongo mpakani mwa Tanzania na Uganda na hakuonekana tena hadi mwili wake ulipoonekana.

Alisema baada ya polisi kuwakamata watuhumiwa watatu kuhusika na mauaji hayo, wananchi walihamasishana huku wakiwa na silaha za jadi na kuchoma nyumba hizo na kufyeka mashamba.

Alisema watu wawili walijeruhiwa katika tukio hilo na wanaendelea na matibabu.



Chanzo: mwananchi.co.tz