Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kijana wa miaka 20 kizimbani kwa unyang'anyi wa kutumia silaha

46566 Pic+kizimbani

Wed, 13 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.  Mkazi wa Gongolamboto Majohe jijini Dar es Salaam, Abdallah Maulid maarufu ‘Mnongano’ (20) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala akikabiliwa na shtaka la unyang'anyi wa kutumia silaha.

Wakili wa Serikali, Grace Lwila leo Machi 13, 2019 alimsomea shtaka hilo Mnongano  mbele ya Hakimu Mkazi, Flora Haule.

Kwa mujibu wa kesi hiyo ya jinai namba 224 ya mwaka 2019 mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha, Julai 20, 2018 kinyume na kifungu cha 287 (A) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Lwila alidai siku hiyo ya tukio, Mnongano akiwa eneo la Majohe kwa Kaisi wilaya ya Ilala aliiba fedha taslimu Sh300,000 na simu ya mkononi aina ya Tecno J8 yenye thamani ya Sh350,000.

Pia aliiba begi jeusi ambalo ndani yake kulikuwa na cheti cha udereva, kadi ya benki ya CRDB, leseni ya udereva, nakala ya kadi ya gari, kadi ya bima na chaji ya simu mali ya Hamis Kalenge.

Iliendelea kudaiwa mahakamani hapo kabla na baada ya mshtakiwa huyo kufanya tukio hilo alitishia kuua kwa kutumia kipande cha nondo ili kujipatia vitu hivyo kwa urahisi.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa alikana na upande wa mashtaka ulieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Hakimu Haule aliiahirisha kesi hiyo hadi Machi 26, 2019 ambapo mshtakiwa huyo atasomewa Maelezo ya awali (PH).

Hata hivyo mshtakiwa huyo alipelekwa rumande kwa sababu shtaka linalomkabili la unyang'anyi wa kutumia silaha ni miongoni mwaka mashtaka yasiyo na dhamana.



Chanzo: mwananchi.co.tz