Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kijana jela miaka 60 kwa kubaka mwanafunzi

Ada6372ae563aa25fffc391b3e29a1de Kijana jela miaka 60 kwa kubaka mwanafunzi

Mon, 23 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAHAKAMA ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora imemhukumu Machiya Shija (24) kutumikia kifungo cha miaka 60 gerezani baada ya kukiri makosa mawili likiwemo la kubaka mwanafunzi wa kidato cha kwanza.

Akitoa hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya hiyo, Eddah Kahindi alisema Mahakama inamhukumu kijana huyo mkazi wa Kata ya Ziba wilayani Igunga kifungo cha miaka 30 kwa kila kosa ili iwe fundisho kwa wengine. Awali Mwendesha Mmashitaka wa Polisi Wilaya ya Igunga, Alex Kataya aliieleza Mahakama kuwa mshitakiwa alikabiliwa na mashitaka mawili. Kataya alisema shitaka la kwanza lilikuwa na kumbaka mwanafunzi kinyume na kifungu 130 (1) (2) (c) na kifungu (131) (1) cha Kanuni ya Adhabu Sura 16 mapitio ya 2019.

Mahakama ilielezwa kuwa, kati ya Machi 5 – 12 mwaka huu usiku katika kijiji cha Mangungu Kata ya Bukoko Shija alifanya mapenzi na mwanafunzi wa miaka 16 anayesoma kidato cha kwanza katika Shule ya sekondari Bukoko. Katika shitaka la pili kijana huyo alidaiwa kumzuia mtoto huyo asiendelee na masomo jambo ambalo ni kinyume na kifungu 60 A (1) (a) na 2 ya Sheria ya Elimu Sura ya 353 iliyofanyiwa mapitio No. 2 ya 2016. Baada ya kusomewa mashitaka hayo Shija alikiri mbele ya Mahakama kutenda makosa hayo.

Hakimu Eddah alisema kwa kuwa mshitakiwa amekiri kutenda makosa hayo pasipo kulazimishwa Mahakama pasipo shaka inamtia hatiani. Kabla hakimu Eddah hajatoa hukumu hiyo, Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Kataya aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Chanzo: habarileo.co.tz