Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kigwangalla asimulia mshtuko wa mawe barabarani usiku

11658 Pic+kigwangala TanzaniaWeb

Wed, 18 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tarime. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema katika dhana ya usalama alishtuka kuona mawe yamepangwa barabarani kuzuia msafara wake.

Juzi saa mbili usiku, Dk Kigwangalla na msafara wake walikuta rundo la mawe yaliyopangwa katikati ya barabara walipokuwa wakitoka ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa).

Mbali ya waziri huyo, wengine waliokuwa katika msafara huo ni mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima; wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa na viongozi wa Serikali na kisiasa wilayani Tarime.

Viongozi hao walikumbana na kadhia hiyo eneo la Karakatonga, Kata ya Kwihancha wilayani hapa.

Tukio hilo lilitokea saa mbili usiku na kuwalazimu viongozi hao kutumia zaidi ya saa moja kuyaondoa mawe hayo barabarani, huku polisi na askari wa hifadhi wakiimarisha ulinzi.

“Nimefanya ziara nyingi za kikazi sehemu mbalimbali nimetatua migogoro mingi, lakini sijawahi kukutana na hili la Tarime la msafara wangu kupangiwa mawe barabarani. Hii imenishtua, lakini namshukuru Mungu tulimaliza na kutoka salama,” alisema Dk Kigwangalla akisimulia tukio hilo.

“Katika dhana nzima ya usalama nilishtuka, hadi sasa najiuliza pengine tusingefika salama iwapo msafara wangu usingekuwa na ulinzi imara na wa kutosha.”

Mawe yalivyoondolewa

Wakati Dk Kigwangalla, Malima na viongozi wengine wakiendelea kuondoa mawe barabarani wakisaidiana na baadhi ya askari, polisi wenye sare na wenzao wa hifadhi walilizunguka eneo hilo wakiwa na silaha.

Baadhi ya watu waliokuwa kwenye msafara huo ghafla walionekana wakiwa na silaha mkononi na baadaye ilibainika kuwa watu hao ni askari kanzu.

Alichojifunza waziri

Dk Kigwangalla alisema ziara na tukio hilo licha ya kumpa mshtuko, limemsaidia kubaini mambo mengi yakiwamo uhusiano mbaya uliopo kati ya mamlaka za hifadhi na jamii inayozizunguka.

Alisema ni lazima hilo lishughulikiwe na kumalizika kwa manufaa ya pande zote mbili.

“Mahusiano mabaya lazima yaishe ili kuleta tija katika sekta ya uhifadhi endelevu unaonufaisha wananchi wanaopakana na hifadhi na Taifa kwa ujumla,” alisema.

Kisha aliongeza, “nimegundua kuwapo masilahi ya kisiasa yanayosababisha migogoro isiyoisha kati ya jamii na hifadhi. Nawasihi wanasiasa wenzangu kuacha tabia hii kwa kuweka mbele masilahi ya Taifa.”

Waziri huyo alisema uhaba wa maeneo kwa ajili ya shughuli za binadamu ikiwamo kilimo, ufugaji na makazi katika sehemu zinazopakana na hifadhi ni miongoni mwa changamoto zinazopaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

“Ndani ya maeneo ya hifadhi kuna ardhi yenye rutuba na malisho. Hii inawavutia baadhi ya wananchi kuingia na kufanya shughuli za kibinadamu hifadhini kinyume cha sheria,” alisema.

Malima asema tukio la ‘kawaida’

Wakati Dk Kigwangalla akielezea kushtushwa na tukio la mawe kupangwa barabarani, mkuu wa mkoa, Malima alisema hilo halikumshangaza kwa sababu ni kati ya mambo anayokumbana nayo mara kwa mara anapofanya ziara maeneo hayo.

“Sikupata wasiwasi wala hofu baada ya kuona mawe barabarani kwa sababu licha ya kuwa na ulinzi imara na wa kutosha kukabiliana na dharura yoyote, pia haikuwa mara yangu ya kwanza kukuta mawe barabarani ninapofanya ziara huku (Tarime),” alisema.

Hata hivyo, alisema mawe ya safari hii yalikuwa mengi na makubwa kulinganisha na siku zingine.

“Hata kamati ya chama iliyoongozwa na waziri mkuu mstaafu, Mizengo Pinda ilipofika Tarime kufuatilia mgogoro huu ilikuta mawe barabarani lakini si mengi na makubwa kama ya safari hii,” alisema Malima. Kamati ya Pinda iliyokuwa na wajumbe wanne; mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Gaudentia Kabaka; mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Kheri James na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Makongoro Nyerere ilifanya ziara wilayani Tarime Juni 2.

Pamoja na kutembelea maeneo yenye mgogoro, kamati ilizungumza na viongozi wa Serikali na CCM wilayani humo na Mkoa wa Mara.

Malima alisema yanapotokea matukio ya aina hiyo, baadhi ya watu huelekeza tuhuma kwa mamlaka za Serikali.

“Wapo wanaowatuhumu baadhi ya wajumbe wangu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama kuhusika kuhujumu misafara ya viongozi wanaofika Tarime kutafuta suluhu ya mgogoro wa mpaka kati ya hifadhi na wananchi, lakini tuhuma hizi si za kweli. Ni wananchi wanaohusika na vitendo hivi,” alisema Malima.

Mgogoro huo umesababisha mvutano na malumbano ya wazi kati ya viongozi wa Serikali na wa kisiasa wilayani Tarime.

Chadema, CCM waungana

Mgogoro wa mipaka wilayani Tarime umewaunganisha viongozi wa CCM na Chadema ambao wanawatetea wananchi.

Kwa nyakati tofauti, wakati wa ziara za viongozi wakiwamo Malima, kamati ya Pinda kabla ya juzi Waziri Kigwangalla, vyama hivyo vinasema hifadhi imewafuata wananchi wanaodai kuishi eneo hilo kwa zaidi ya miaka 50.

“Mipaka inayodaiwa na watu wa hifadhi si halali kwa sababu imesogezwa hadi kwenye maeneo ya vijiji kwa mujibu wa vigingi vilivyowekwa mwaka 1968 ambavyo viko kilomita nane ndani ya hifadhi,” alisema mwenyekiti wa UVCCM wilayani Tarime, Godfrey Francis akimweleza Dk Kigwangalla.

Kauli kama hiyo ilitolewa na mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche aliyesema mgogoro unatokana na viongozi wa Serikali kushirikiana na hifadhi kuweka alama mpya za mipaka bila kuwashirikisha wananchi.

Dk Kigwangalla alikubaliana na hoja ya kuwaacha wananchi ambao licha ya kuwa ndani ya eneo la wazi (buffer zone), lakini wamekingwa na milima inayozuia mwingiliano wa watu na wanyamapori. Alitaka waachwe waendelee na shughuli zao eneo hilo.

Kwa walio ndani ya hifadhi na eneo la wazi linalofikiwa na wanyamapori, waziri huyo aliwapa miezi mitatu wawe wameondoka kwa hiari kabla ya kuondolewa kwa nguvu na mali zao kuharibiwa na kutaifishwa.

Katika ziara hiyo, Dk Kigwangalla aliagiza katibu wa UVCCM wilayani Tarime, Newton Mongi na mjumbe wa Kamati ya Siasa ya chama hicho wilayani hapa, Richard Tiboche kutiwa mbaroni wakidaiwa kuitukana Serikali.

Chanzo: mwananchi.co.tz