Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kigogo wizara ya ardhi alivyotoa ushahidi kesi ya Gugai wa Takukuru

73066 Gugai+pi

Tue, 27 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kamishna Msaidizi wa kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Nathaniel Mathew (47), ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa anamfahamu aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa Takukuru, Godfrey Gugai kama mmiliki wa viwanja viwili vilivyoko Mbweni JKT na Bunju, jiji Dar es Salaam.

Mathew ambaye ni shahidi wa 23, katika kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zilizozidi kipato chake, inayomkabili Gugai na wenzake watatu, ameeleza hayo jana Jumatatu Agosti 26,2019 wakati akitoa ushahidi dhidi ya Gugai.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Awamu Mbagwa akisaidiana na Ipyana Mwakatobe na Estazia Wilson, Mathew alidai  alimfahamu Gugai baada ya kupokea barua Novemba 2018 kutoka ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( Takukuru), wakitaka taarifa kuhusu uhalali wa umiliki wa viwanja hivyo.

Akitoa ushahidi wake, mbele ya hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, shahidi huyo alidai baada ya kupokea barua hiyo, walianza kufanya uchunguzi na kubaini Gugai alikuwa anamiliki viwanja viwili katika eneo hilo.

"Kiwanja namba 225 kitalu 6 kilichoko Mbweni JKT na kiwanja namba 150 kitalu 8 ambacho kipo Bunju, Dar es Salaam," alidai shahidi.

Kamishna huyo alidai katika uchunguzi wao, waligundua kulikuwa na barua ya maombi ambayo alimwandikia Kamishna kama muombaji wa viwanja namba 63 na 64 kitalu C, kilichoko  eneo la Ununio.

Pia Soma

Viwanja hivyo alikuwa tayari anavimiliki mwenyewe ila alitaka  umiliki kihalali.

“Baada ya kubaini hilo, tuliwasilisha vielelezo ambavyo ni kopi za mauziano ambazo zilikuwa kumbukumbu kwenye majalada na majalada tuliyaweka hadi leo (jana) ambapo nimemkabidhi Wakili wa Serikali," alidai Mathew.

Shahidi huyo aliendelea kudai kuwa kiwanja namba 150 kitalu 8, alianza kumiliki Januari Mosi, 2008 ambapo aliuziwa na Serikali kwa gharama ya Sh3.6 milioni.

“Pia katika kiwanja namba 225 kitalu 6, alipata umiliki kwa njia ya mauziano kutoka kwa Angela Kiziga kwa gharama ya Sh3.5 milioni, lakini kiwanja hiki kabla ya kuuziwa Gugai, Kiziga alikuwa anakiuza kwa Sh8 milioni,”alidia

Baada ya maelezo hayo shahidi aliomba Mahakama ipokee hati za viwanja hivyo kama vielelezo katika kesi hiyo.

Mahakama hiyo ilipokea vielelezo hiyo na Hakimu Simba aliahirisha kesi hadi leo itakapoendelea na ushahidi wa upande wa mashtaka.

Tayari mashahidi 23 wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya Gugai.

Miongoni mwa mashahidi hao ni kikongwe, Amina Kilemba(81) ambaye aliieleza mahakama hiyo kuwa yeye ndio aliyemuuzia Gugai kiwanja namba 64 kilichopo eneo la Boko Ununio kwa gharama ya Sh80 milioni.

Kilemba alidai kiwanja hicho kilikuwa ni cha mwanae aitwaye  Mize Kilemba, ambaye ameshafariki dunia.

Mbali na Gugai, washitakiwa wengine katika kesi hiyo  ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali, linamkabili Gugai.

Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na kipato chake, ambapo anadaiwa kutenda  kosa hilo kati ya Januari 2005 na Desemba, 2015.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz