Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kigogo wa Takukuru kizimbani

49500 Pic+takukuru

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Aliyekuwa mkurugenzi wa mipango, ufuatiliaji na tathmini wa Takukuru, Kulthum Mansoor (57) amepandishwa kizimbani akikabiliwa na makosa nane, ikiwa ni siku moja baada ya Rais John Magufuli kuzungumzia suala lake.

Kati ya mashtaka aliyosomewa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ni la utakatishaji Sh1.477 bilioni, kosa ambalo halina dhamana.

Akizungumza wakati wa hafla ya kumuapisha balozi wa Tanzania nchini Cuba, Valentino Mlowola juzi, Rais Magufuli alionyesha kushangazwa na jinsi ambavyo vyombo vya dola havijamfikisha mahakamani kigogo huyo wa Takukuru licha ya kuwauzia viwanja hewa wafanyakazi wa taasisi hiyo.

Alisema Takukuru ni kwa ajili ya kila mwananchi hata wafanyakazi wa taasisi hiyo na haikuchukua muda kabla ya kukamatwa juzi jioni na kufikishwa mahakamani jana.

Kulthum, akionekana mwenye uso uliopoa, aliingia mahakamani hapo akiwa amevalia baibui jeusi, ushungi wa maziwa na miwani huku akisindikizwa na askari wa kike.

Wakili wa Serikali, Simon Wankyo alidai mbele ya Hakimu Mfawidhi Kelvin Mhina kuwa Kulthum ameshtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi.

Wankyo alidai katika kosa la kwanza la kughushi, kati ya Januari 2013 na Mei 2018 akiwa makao makuu ya Takukuru jijini Dar es Salaam, alitoa barua ya ofa ikionyesha imetoka katika Halmashauri ya Bagamoyo mkoani Pwani.

Alidai kosa la pili hadi la saba, ni mtuhumiwa kupokea viwango tofauti vya fedha kutoka kwa watumishi wa Takukuru kama malipo ya viwanja vilivyopo kijiji cha Ukuni wilayani Bagamoyo huku akionyesha kuwa yeye ndiye mmiliki.

Katika kosa la nane la utakatishaji wa fedha, ilidaiwa kuwa kati ya Januari mwaka 2013 na Mei 2018 akiwa eneo la Upanga jijini Dar es Salaam alijipatia Sh1.477 bilioni huku akijua fedha hizo ni zao la makosa mengine.

Mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za aina hiyo. Wankyo alidai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo aliiomba mahakama hiyo ipange tarehe ya kuitaja.

Hakimu Mhina aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 12.

Awali jana asubuhi, naibu mkurugenzi wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo aliwaambia waandishi wa habari akiwa makao makuu ya ofisi hizo zilizoko Upanga, takriban kilomita 3 kutoka Mahakama ya Kisutu, mambo waliyoyabaini kuhusu malalamiko hayo.

“Tulipata malalamiko mengi kutoka kwa watumishi wa Takukuru. Baada ya malalamiko hayo hatua zilianza mara moja,” alisema Brigedia Mbungo.

Alisema katika uchunguzi huo walibaini mambo saba, likiwemo la viwanja vilivyoahidiwa kuuzwa ambavyo ni zaidi ya 300 na fedha alizokuwa ameshalipwa na watumishi kwa ajili ya kuvinunua.

Alisema waligundua mtuhumiwa alijipatia fedha nyingine zaidi ya Sh200 milioni ambazo alilipwa na watumishi kama gharama kwaajili ya hati na nyaraka nyingine za umiliki.

Brigedia Mbungo alisema pia walibaini fedha hizo hazikuwahi kuwasilishwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya malipo ya hati na tozo za ardhi.

Katika uchunguzi huo, kwa mujibu wa Brigedia Mbungo, walibaini kuwa viwanja vilivyokuwa vinazungumziwa havikuwa vya mtuhumiwa.

Alisema Wizara ya Ardhi imethibitisha kuwa Kulthum si mmiliki halali wa viwanja vilivyokuwa katika mazungumzo ya kuuzwa na kwamba nyaraka alizokuwa akidai zinahalalisha umiliki wake katika hiyo ardhi ni za kughushi.

Alisema baada ya kufanya uchunguzi, Takukuru ilimsimamisha kazi tangu Machi 8 mwaka jana kutokana na tuhuma hizo.

Brigedia Mbungo alitoa wito kwa watendaji wa Serikali kubadili mwelekeo wa maisha na kuhakikisha wananchi hawadhulumiwi mali zao.

“Watumishi wa Serikali na wanaofanya kazi kwenye mashirika na taasisi za umma wawe waaminifu na wajipatie fedha kihalali,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz