Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kigogo mstaafu serikalini ahojiwa uhujumu

90247 Mstaafu+pic Kigogo mstaafu serikalini ahojiwa uhujumu

Mon, 30 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi/Dar. Kikosi kazi kilichoundwa na Serikali kupambana na ujangili nchini, kimemtia mbaroni mkurugenzi mtendaji wa zamani wa mfuko wa uwekezaji Tanzania (UTT), Dk Hamis Kibola.

Dk Kibola amewahi kushika nyadhifa za juu katika taasisi mbalimbali za Serikali na alikuwa mtendaji mkuu wa Mamlaka ya Mitaji na Masoko na pia Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE).

Mbali na nyadhifa hizo, aliwahi kuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Shirika la Bima la Taifa (NIC) na ndiye muasisi wa mafanikio ya UTT hadi ikaanzisha kampuni tatu tofauti.

Hata hivyo, tuhuma dhidi yake hazina uhusiano na ofisi alizowahi kuhudumia, bali zinatokana na ukiukwaji wa sheria za uwindaji. Kibola anamiliki kitalu cha uwindaji kilichopo Simanjiro.

Baadhi ya ndugu wamegoma kuzungumzia suala hilo, lakini vyanzo mbalimbali vimelidokeza gazeti hili kuwa Dk Kibola alikamatwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam sambamba na ndugu yake mwingine anayetajwa kuwa na taaluma ya uwindaji wa kimataifa.

“Mimi ninavyofahamu alikamatwa Jumatano iliyopita (Desemba 18,2019) Dar es Salaam na watu waliojitambuliusha ni task force (kikosi kazi) na sifahamu zaidi ya hapo,” alidokeza mmoja wa watu walio karibu naye.

Waziri Kigwangala afunguka

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla alithibitisha kukamatwa kwa Dk Kibola akisema kikosi kazi kinaendelea na mahojiano kuhusu tuhuma zinazomkabili.

“Ni kweli Dk Hamis Kibola owner (mmiliki) wa kampuni ya uwindaji wa kitalii ya HSK alikamatwa na task force na kuwekwa ndani kuanzia tarehe 19.12.2019,” alisema Dk Kigwangalla.

Hata hivyo Dk Kigwangalla alisema Dk Kibola aliachiwa kwa dhamana Desemba 25,2019 na kutakiwa kuendelea kuripoti ingawa hakusema anatakiwa kuripoti kituo gani.

Waziri Kigwangalla alisema mtuhumiwa anahojiwa kwa makosa yanayodaiwa kufanyika wakati wa uwindaji kwenye kitalu cha Simanjiro GCA West kilichopo Simanjiro mkoa wa Manyara.

Alitaja makosa anayotuhumiwa kuyafanya yeye au kampuni yake kuwa ni pamoja na kuwinda wanyama zaidi ya walioruhusiwa kwenye kibali alichopewa, kuwinda majike na kukwepa kodi na kuisababishia Serikali hasara.

Chanzo: mwananchi.co.tz