Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kigogo mabasi ya mwendokasi mgonjwa, kesi yake yakwama

50283 Pic+kisena

Thu, 4 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa  Kampuni ya Huduma za Usafirishaji wa Mabasi yaendayo Haraka maarufu ‘Mwendokasi’ (Udart), Robert Kisena leo ameshindwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kile kilichoelezwa kuwa ni mgonjwa.

Pia mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo, Chen Shi ambaye ni raia wa China naye ni mgonjwa na ameshindwa kufika mahakamani hapo. 

Kisena na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka 19 yakiwamo ya utakatishaji fedha katika kesi ya uhujumu uchumi.

Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Iman Nitume leo aliieleza Mahakama mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa amepewa  taarifa kutoka gerezani kuwa Kisena na Chen ni wagonjwa na kwamba wameshindwa kufikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza kesi yao.

Alieleza kuwa kesi hiyo leo ilikuwa ni kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

"Bado tunaendelea na uchunguzi katika kesi hii, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," alitoa ombi.

Baada ya kueleza hayo, wakili wa utetezi, Semi Malimi ameomba upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi kwa wakati ili kesi hiyo iweze kuendelea na hatua nyingine.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 17 itakapotajwa.

 

Mbali na Robert Kisena, washtakiwa wengine ni Kulwa Kisena pamoja na mhasibu wa kampuni hiyo, Charles Selemani Newe.

Kati ya mashtaka hayo 19 yanayowakabili washtakiwa hao; shitaka moja ni kuongoza mtandao wa uhalifu; mashtaka manne ya kughushi nyaraka; manne ya  kuwasilisha nyaraka za uwongo na manne ya utakatishaji fedha zaidi ya Sh2.4 bilioni.

Mashtaka mengine ni kujenga kituo cha mafuta bila kibali cha Shirika la Maendeleo ya Petroli (TBDC) na kuuza mafuta mahali pasiporuhusiwa (makao makuu ya kampuni hiyo- Jangwani).

Mashtaka mengine ni  kujipatia pesa kwa njia za udanganyifu zaidi ya Sh1.1 bilioni; kuisababishia Udart hasara ya zaidi Sh2.4 bilioni na wizi wa mafuta yenye thamani ya zaidi ya Sh1.2 bilioni mali ya Udart.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Januari Mosi 2011 na Mei 2018 katika ofisi za kampuni hiyo zilizoko eneo la Jangwani, wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam.



Chanzo: mwananchi.co.tz