Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kigogo apandishwa kizimbani akidaiwa kumpa rushwa Lukuvi

9851 Pic+lukuvi TanzaniaWeb

Fri, 3 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imempandisha kizimbani mkurugenzi wa Kampuni ya Kiluwa Steal Group Limited, Mohamed Kiluwa (50) kwa tuhuma za kutoa rushwa ya Sh90 milioni kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi.

Mshtakiwa huyo ambaye pia ni mkurugenzi wa Kampuni ya Kiluwa Free Processing Zone alipandishwa kizimbani jana mbele ya hakimu mkazi mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Huruma Shaidi na kusomewa shtaka moja la kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Akimsomewa shtaka hilo, wakili wa Serikali mkuu kutoka Takukuru, Maghela Ndimbo alidai kuwa Julai 16 kati ya saa sita mchana na saa nane mchana mshtakiwa huyo alitoa Dola 40,000 (sawa na Sh90 milioni) kwa Waziri Lukuvi.

Wakili Ndimbo alidai mshtakiwa huyo alitoa fedha hizo ili asiwasilishe hati za umiliki wa kiwanja namba 57 Block B Kikongo na D Disunyura vilivyopo eneo la viwanda Kibaha mkoani Pwani.

Wakili Ndimbo aliiomba Mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kesi hiyo na kuongeza kuwa upelelezi bado unaendelea na hawana pingamizi kuhusiana na kutoa dhamana kwa mshtakiwa.

Wakili wa utetezi, Imani Madega aliomba mteja wake apatiwe dhamana kwa kuwa upande wa mashtaka hauna pingamizi.

Hakimu Shaidi alisema dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo ipo wazi, hivyo anatakiwa kuwa na wadhamini wawili mmoja atoe fedha taslimu mahakamani Sh45 milioni au awasilishe hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiwango hicho cha fedha.

Masharti hayo yalitekelezwa na upande wa utetezi na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Agosti 15 mwaka huu.

Chanzo: mwananchi.co.tz