Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kigogo Takukuru aandika barua kwa DPP kukiri makosa

82573 Pic+takukuru Kigogo Takukuru aandika barua kwa DPP kukiri makosa

Sat, 2 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mchunguzi Mkuu wa  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Cosmas Batanyita amemuandikia barua mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP) kuomba msamaha na kukiri makosa.

Batanyita ameeleza hayo leo Ijumaa Novemba Mosi, 2019 kesi yake ilipotajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka saba likiwemo la kuomba rushwa ya Sh200 milioni na kutakatisha fedha.

"Nimeandika barua ya kukiri na kuomba msamaha kwa DPP, hivyo naomba kujua maombi yangu yamefikia hatua gani," amedai mshtakiwa huyo.

Batanyita baada ya kueleza hayo wakili wa Serikali, Gloria Mwenda amedai upelelezi haujakamilika na kwamba hana taarifa kuhusu  mshtakiwa huyo kuandika barua.

" Sina taarifa kama mshtakiwa amemuandikia barua DPP naomba  niwasiliane na mkuu  wa waendesha mashtaka hapa Kisutu, Wankyo Simon kuhusu hiki alichoongea  mshtakiwa,” amedai wakili Mwenda. Akijibu hoja ya mshtakiwa, Simon amesema maombi yake yanafanyiwa kazi na yakikamilika atapewa taarifa.

Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, Hakimu mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kelvin Mhina ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 15, 2019 itakapotajwa.

Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na mashtaka ya kutakatisha fedha yanayomkabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Mshtakiwa alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Agosti 9, 2019 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 76/2019.

Kati ya mashtaka hayo saba, matatu ni ya kushawishi rushwa, moja la kuomba na kupokea rushwa na mashtaka matatu  ya kutakatisha fedha.

Katika kesi ya msingi, Batanyita akiwa mwajiriwa wa Takukuru anadaiwa Februari 9, 2019 katika eneo la Upanga alishawishi na kuomba rushwa  ya Sh200 milioni kutoka kwa Hussein Gulamal Hasham ili aweze kuharibu ushahidi katika kesi ya ukwepaji wa kodi ilivyokuwa inamkabili Husein wakati akijua  kuwa upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa unaendelea Takukuru.

Anadaiwa Februari 10, 2019 katika eneo la Sabasaba, Batanyita alijipatia Dola 20,000  za Marekani kutoka kwa Faizal  Hasham ikiwa ni ahadi ya kuharibu ushahidi katika kesi ya ukwepaji kodi inayomkabili Hussein Hasham, wakati akijua upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa unaendelea.

Chanzo: mwananchi.co.tz