Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kigogo Halmashauri Chato, madiwani CCM mbaroni kwa uvuvi haramu

28989 Samaki TanzaniaWeb

Tue, 27 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Geita. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita, Bathromeo Manunga na madiwani wawili wa CCM wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kujihusisha na uvuvi haramu, kutozwa faini ya zaidi ya Sh21 milioni.

Ofisa mfawidhi ulinzi na usimamizi wa uvuvi Kanda ya Ziwa Victoria, Didas Mtambalike amesema leo Jumatatu Novemba 26, 2018 kuwa viongozi hao walikamatwa kwa nyakati tofauti kati ya Novemba 2 hadi 22, 2018.

Mtambalike amesema Manunga alikamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na kumiliki zana haramu katika mwalo la Bwongera wilayani Chato.

Amesema Manunga alikutwa na nyavu 56 zilizopigwa marufuku kutumia kuvua samaki na nyingine 121  zilizounganishwa, injini tano na  boti, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh7.9 milioni.

"Baada ya kufikishwa polisi watuhumiwa walikiri makosa yao na kutozwa faini kwa mujibu wa sheria," amesema Mtambalike.

Mtambalike amesema watuhumiwa hao walitiwa mbaroni na kikosi maalum cha  operesheni Sangara Mkoa wa Geita,

Katika operesheni hiyo diwani wa Bwina, Sospeter Nyamang'ondi nae alikamatwa na kutozwa faini ya Sh2 milioni kwa kukutwa na nyavu haramu huku mwenzake wa kata ya Muganza, Emmanue Tagota akitiwa mbaroni kwa kumiliki nyavu zenye ukubwa chini ya milimita 6,86 zenye thamani ya zaidi ya Sh 3.6 milioni na kutozwa faini ya Sh10 milioni.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz