Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kifo cha profesa chuo cha Muhimbili chazua utata

15080 Professa+pic TanzaniaWeb

Sun, 2 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Profesa wa Chuo Kikuu Kishiriki Muhimbili (Muhas), Emil Kikwilu amefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha baada ya mwili wake kukutwa karibu na nyumbani kwake ukiwa na majeraha kichwani.

Msemaji wa familia ya marehemu, Zenodi Shauritanga leo Jumamosi Septemba Mosi, 2018 ameieleza MCL Digital kuwa mwili wa msomi huyo  uliokotwa Agosti 27, 2018 ukiwa hatua 15 kutoka nyumbani kwake.

Mwili wa Profesa huyo uliagwa katika viwanja vya chuo hicho jana Agosti 31, 2018 na kuzikwa nje ya nyumba yake, Kimara jijini Dar es Salaam.

“Tuliona mwili kati ya saa tatu usiku wa siku hiyo, ulikuwa na majeraha makubwa kichwani ni kama vile alikatwa,” amesema Shauritanga.

“Niliitwa na kushuhudia na baadaye polisi walifika wakauchukua mwili na kuupeleka mochwari katika hospitali ya Taifa Muhimbili.”

Amesema alifariki dunia wakati akirejea nyumbani akitokea kazini, kwamba hakukutwa na simu, begi alilokuwa akiweka kompyuta mpakato na vyombo vyake alivyokuwa akiweka chakula.

“Tulikuta mwili kwenye kichochoro sehemu ambayo gari wala pikipiki haviwezi kupita. Hatujui kilitokea nini tunasubiri taarifa za uchunguzi wa polisi,” amesema Shauritanga.

Akizungumza na MCL Digital Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Jumanne Murilo amesema walipata taarifa kuhusu tukio hilo na kwamba wanaendelea na uchunguzi kwa kuwa kifo hicho kina utata.

"Tunachunguza ili kujua sababu za kifo chake, tukikamilisha tutaijulisha familia yake," amesema.

 

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz