Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kichanga cha siku moja chaokotwa ndani ya mfuko wa rambo

Wed, 17 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Mtoto mchanga mwenye jinsia ya kiume mwenye umri wa siku moja ameokotwa akiwa hai na wasamaria wema baada ya kutupwa na mama yake muda mfupi baada ya kuzaliwa eneo la Kilakala Mzambarauni manispaa ya Morogoro.

Akizungumzia tukio hilo le, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa amesema mtoto huyo aliokotwa Aprili 15 majira ya asubuhi akiwa amefungwa kwenye mfuko wa plastiki.

Amesema kuwa baada ya kuokotwa mtoto huyo alipelekwa katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas kwa ajili ya kupewa chanjo mbalimbali pamoja na uangalizi wa karibu huku juhudi za kumsaka mama aliyemzaa na kumtupa zikiendelea.

Katika tukio jingine, watoto watatu wamefariki dunia katika matukio tofauti mkoani hapa baada ya kuzama kwenye maji wakati wakiogelea.

Tukio la kwanza, Kamanda Mutafungwa amesema lilitokea Aprili 15 saa 9:00 alasiri katika kijiji cha Mngeta –Ifakara wilaya ya Kilombero, ambapo watoto wawili, Lumbango Kurwa (5) na Mussa Alfonce (4) walifariki dunia baada ya kuzama kwenye dimbwi la maji lenye kina kirefu wakati wakicheza kwenye dimbwi hilo.

Alisema miili ya watoto hao imeshakabidhiwa kwa ndugu baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu.

Kamanda Mutafungwa alisema tukio jingine lilitokea Aprili 15 saa 10:00 alasiri kata ya Luhungo manispaa ya Morogoro, ambapo mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya sekondari Sua, Baraka Jacobo (17) alifariki dunia baada ya kuzama kwenye korongo wakati akiogelea.

Mwili wa mwanafunzi huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.

Kamanda Mutafungwa ametoa tahadhari kwa watu wanaoishi jirani na mito na makorongo hasa katika kipindi hiki cha mvua kuwa makini wanapovuka ama kuoga ili kuepuka ajali za kuzama maji.



Chanzo: mwananchi.co.tz