Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kibatala ashindwa kumhoji shahidi wa saba kesi ya kina Mbowe

75112 Mbowepic

Tue, 10 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Peter Kibatala, wakili wa utetezi katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema, akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ameshindwa kumhoji shahidi wa saba wa upande wa mashtaka.

Shahidi huyo, Victoria Wihenge (34) ambaye ni ofisa uchaguzi kutoka manispaa ya Kinondoni, hakuhojiwa kwa kile alichodai kuwa wenzake wakati wanamhoji yeye hakuwepo,.

Kibatala amedai  wakati mawakili mwenzake wanamhoji Wihenge, yeye hakuwepo na ili asirudie ambacho wenzake wamemuuliza shahidi huyo, ameona hana jambo lolote la kumuuliza, hivyo upande wa utetezi kufunga ukurasa wa kumhoji.

Kibatala ameeleza hayo leo Jumanne Septemba 10, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya upande wa utetezi kumalizia kumhoji shahidi wa upande wa mashtaka.

Wakili huyo alitakiwa kumhoji shahidi kutokana na ushahidi alioutoa mahakamani hapo kuhusu kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi hao.

Kibatala baada ya kuileza mahakama hiyo, upande wa mashtaka ulimhoji shahidi huyo baadhi ya maswali aliyokuwa ameulizwa na upande wa utetezi na baada ya hapo aliruhusiwa  kuondoka katika chumba cha mahakama baada ya kumaliza kutoa ushahidi.

Pia Soma

Advertisement
Baada ya hapo aliitwa shahidi wa nane wa upande wa mashtaka  Bernad Nyambari ( 42)ambaye alianza kutoa ushahidi wake dhidi ya washtakiwa hao.

Nyambari ni Mkuu wa Upelelezi wa  Wilaya ya Kipolisi ya Mbagala.

Hata hivyo, wakati shahidi huyo akiendelea kutoa ushahidi wake wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alisimama mahakamani na kuiomba  iahirishwe kwa muda ili mawakili wa pande zote mbili kujadili jambo.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo kwa muda ili kupisha majadiliano baina ya mawakili wa pande zote.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mbunge waTarime Mjini (CCM), Esther Matiko;   Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; naibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar); mbunge wa Kawe, Halima Mdee; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 13 katika kesi ya jinai namba 112/2018.

Chanzo: mwananchi.co.tz