Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kibatala afunguka kukamatwa ofisa TRC aliyefukuzwa kazi kwa kupinga tozo

Kibatalapiic Data Kibatala afunguka kukamatwa ofisa TRC aliyepinga tozo

Sat, 27 Aug 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Peter Kibatala, Wakili anayemtetea Jonas Afumwisye, aliyekuwa Ofisa wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) amesema, mtumishi huyo aliyefukuzwa kazi, amekamatwa na Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Afumwisye alifukuzwa kazi Agosti 19, 2022 na Bodi ya TRC kwa madai ya kupinga tozo za miamala ya simu kwenye makundi ya kijamii.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa alimwandikia barua Afumwisye kumjulisha kuhusu uamuzi huo Agosti 19 baada ya kuthibitika kwa tuhuma zilizokuwa zikimkabili.

Mara baada ya uamuzi huo, Wakili Peter Kibatala alikuwa miongoni mwa waliojitokeza kutangaza kumtetea kukata rufaa kupinga hatua hiyo akidai haki dhidi ya mtumishi huyo haikutendeka.

Jana Ijumaa, Agosti 26, 2022, Kibatala akizungumza na alisema, “Jana (juzi) tulikamilisha rufaa yetu dhidi ya uamuzi wa kinidhamu wa ndani wa TRC uliosababisha mteja wangu kufukuzwa kazi.”

Amesema licha ya muda wa kukata rufaa kuwa siku 45 tangu alipopokea barua, “na kwa sababu za kimgogoro wa kisheria, tumekata mapema rufaa na kuwapelekea nakala mkurugenzi mkuu wa TRC ambaye ndiye alisaini ile barua ya kumfukuza kazi.”

Aidha, amesema barua hiyo imepelekwa kwa bodi hiyo na “rufaa mama imepelekwa Dodoma kwa ajili ya kuwasilisha Jumatatu kwa Tume ya Utumishi wa Umma.”

Kuhusu kukamatwa amesema, “Leo (jana) amenipigia simu mteja wangu kuwa amefuatwa nyumbani kwake na watu wawili waliojitambulisha ni maofisa wa polisi kutoka Central.

“Nikamweleza kwa mujibu wa PGO hao wanapaswa kujitambulisha majina yao, wakuonyeshe vitambulisho, vyeo vyao na hata namba zao za U-polisi.

“Hii ni kwa mujibu wa sheria na kanuni ambazo hazina ukakasi wowote, nikamuuliza hayo maswali wamekujibu akasema hapana,” amesema Kibatala.

Amesema lengo la masharti hayo ni kuweka uwazi, “ili mtu kama ana mke, mme au ndugu ampe taarifa kwamba anapelekwa wapi, sasa unaposhindwa kumweleza, ndugu zake wamtafutaje?”

Kibatala amesema, baada ya muda simu ya mteja wake ikawa haipatikani na akachukua jukumu la kuwapigia simu maofisa wa Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na wakamjibu, “ni kweli kuna mtu kama huyo na wakaeleza anatuhumiwa kuchapisha taarifa zisizo sahihi kwa njia ya mtandao.

“Sasa angalau mteja wangu nimefahamishwa anatuhumiwa kwa tuhuma hizo. Kwa sasa taarifa ni hizo na kama kutakuwa na zingine tutawasiliana,” amesema Kibatala

Aidha amesisitiza, “toka mara ya kwanza niliposema tutamtetea na tutafanya hivyo si kwenye rufaa yake tu bali kwenye mambo yote ya maslahi ya kisheria, tutapigania kwa mujibu wa sheria inapatikana na hata kama anatuhumiwa kwa tuhuma hizo wamhoji na kuchunguza na kumpeleka mahakamani, tutakuwa naye.”

“Tutawekeza nguvu kwenye rufaa na hiki ambacho kimetokea na lolote ambalo litajitokeza mbele yake,” amesema Kibatala.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alipoulizwa kuhusu mtumishi huyo kushikiliwa kituoni kwake ambapo amesema hayupo ofisini na kumpa mwandishi namba ya kupiga kuulizia hilo.

Namba hiyo ambayo ni ya ofisi ya Kanda hiyo ilivyopigwa, muhusika alijibu hana taarifa na jambo hilo na kumtaka mwandishi ampe muda alifuatilie kwa kuwa naye amekuwa nje ya ofisi tangu asubuhi na kuahidi kumrudia baadaye.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz