Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kibarua mbaroni akituhumiwa kumuua mwajiri akidai malipo

956589b8edc5552046cbcf728f9f3189 Kibarua mbaroni akituhumiwa kumuua mwajiri akidai malipo

Thu, 24 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limekamata watu watatu kwa tuhuma za mauaji mmoja akiwa ni mtumishi wa shambani anayedaiwa kumuua mwajiri wake na mwingine ni mume anayetuhumiwa kumuua mkewe.

Taarifa ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei kwa vyombo vya habari jana, ilimtaja Emmanuel Patsonmwesa mwenye umri wa miaka 22 anayedaiwa kumuua mwajiri wake, Asumwisye Lufingo (Mwambonike) mwenye umri wa miaka 37, mkazi wa Kijiji cha Isangawana wilayani Chunya mkoani Mbeya.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mauaji yalifanyika Januari 2, mwaka huu na Patsonmwesa alikamatwa Machi 21 mwaka huu saa 11 jioni baada ya polisi wa mkoani Mbeya kushirikiana na wa mkoani Songwe kufanya msako mjini Tunduma wilayani Momba, ambako alikamatiwa.

Ilielezwa kwamba Januari 2, mwaka huu saa 10 jioni, Lufingo alikuwa shambani na vibarua wake wawili, Patsonmwesa na mwenzake ambaye jina lake limehifadhiwa. Shamba hilo lipo katika Kijiji cha Isangawana, Kata ya Matwiga, Tarafa ya Kipembawe wilayani Chunya.

Kamanda Matei alisema vibarua hao walimvamia na kumuua bosi wao kwa kumkata kwa panga kichwani ikidaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni madai ya fedha ya ujira wa kulima.

Alisema vibarua hao waliondoka kwa pikipiki ya Lufingo yenye namba za usajili MC 776 BES aina ya Fekon.

Matei alisema polisi wanaendelea kumtafuta mtuhumiwa mwingine aliyeshirikiana na Patsonmwesa.

"Wakati msako unaendelea kumtafuta mtuhumiwa mwingine, bado pikipiki nayo haijapatikana hivyo mahojiano na mtuhumiwa aliyekamatwa yanaendelea ili kubaini ilipo pikipiki ya marehemu waliyoondoka nayo mara baada ya kufanya tukio hilo," alisema katika taarifa hiyo.

Kuhusu aliyemuua mkewe, Kamanda Matei alisema wamemkamata Safari Luwole (43) akidaiwa kumuua Tumaini Anton (45) Februari 4, mwaka huu.

Mtuhumiwa huyo mkazi wa Kijiji cha Horongo, alikamatwa Machi 20 saa 7 mchana kutokana na msako wa polisi katika Kijiji cha Shitete, Kata ya Iwindi Tarafa ya Usongwe wilaya na Mkoa wa Mbeya.

Kamanda alisema Tumaini alikutwa amekufa nyumbani kwake katika Kijiji cha Inolo, Kata ya Iwindi. Inadaiwa mumewe alimuua kwa kumpiga kwa kitu kizito kwenye paji la uso, chanzo kikidaiwa kuwa ugomvi wa kifamilia.

"Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria," alisema Kamanda Matei.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live