Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kibali cha mashahidi chakwamisha kesi ya Gugai

Fri, 22 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeshindwa kuendelea na usikilizaji wa kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zilizozidi kipato chake, inayomkabili aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai, kwa kuwa kibali cha kuwaita mashahidi kutoka mikoani kimechelewa.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Vitalius Peter amedai leo Jumatano, Februari 20, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa.

Peter amedai waliomba kibali cha kuwaita mashahidi wanne kutoka mikoani lakini wamepata taarifa leo kuwa kibali hicho kimekwishatolewa leo (hela ya kuwalipa mashahidi imeshapatikana).

"Ili shahidi aweze kutoa ushahidi akiwa anatokea mkoani ni lazima kipatikane kibali kwa sababu atatakiwa kulipwa, hivyo kibali tulichoomba, leo ndio kimejibiwa sasa tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na ushahidi," amedai Peter.

Wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa aliuomba upande wa mashitaka kuwataja mashahidi watakaowaleta ili kuweka kumbukumbu sawa kuwa asipokuja mmoja aletwe shahidi mwingine.

Akijibu hoja hiyo, Wakili Peter alidai hawawezi kutaja majina ya mashahidi hao ila mahakama itambue kuwa mashahidi watatu wanatoka Mwanza na shahidi mmoja anatokea Musoma.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba aliutaka upande wa mashitaka uhakikishe unaleta mashahidi ili kesi hiyo iweze kuendelea.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 4 na 6, mwaka huu kwa ajili ya kuendelea na ushahidi kwa upande wa mashitaka.

Tayari mashahidi sita wa upande wa mashitaka wameshatoa ushahidi wao wakiwemo Msajili wa Hati Msaidizi, kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Joanitha Kazinja.

Mbali na Gugai, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.

Katika kesi ya msingi, Gugai na wenzake, wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali, ambalo linamkabili Gugai.

Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na kipato chake, ambapo anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari 2005 na Desemba 2015.

Inadaiwa kuwa akiwa Takukuru Dar es Salaam, Gugai alikuwa akimiliki mali za zaidi ya Sh3.6 bilioni, ambazo hazilingani na kipato chake huku akishindwa kutoa maelezo ya mali hizo.



Chanzo: mwananchi.co.tz