Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi za wanawake kuwapiga waume wao zaongezeka Lindi

37758 Pic+kesi Kesi za wanawake kuwapiga waume wao zaongezeka Lindi

Tue, 22 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ruangwa, Lindi. Kina mama wilayani Ruangwa mkoani Lindi hasa katika Kata ya Likunja wamelalamikiwa kuwashushia vipigo waume wao.

Hayo yamesemwa jana katika semina ya mafunzo iliyoandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) na Wizara ya Afya kwa wajumbe wa kamati za ulinzi zitakazosimamia ukatili wa kijinsia katika kata hiyo.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, mtendaji Kata ya Likunja, Hassan Abdallah alisema kesi nyingi zinazofikishwa kwake ni za wanaume kulalamika kupigwa na wake zao.

Kwa mfano, alisema kuanzia Juni hadi Desemba mwaka jana alipokea zaidi ya kesi saba za kina mama kuwashushia vipigo waume zao.

“Hii yote ni kutokana na mila ya mama kuwa kichwa cha familia. Wanawake wanakuwa na nguvu sana kiasi cha kuwadhibiti wanaume,” alisema.

“Mimi najua mengi jamani na hizi kesi sio kwamba wanaume wanakuwa wamelewa hapana, wanakuwa wazima kabisa.”

Mkazi wa Likunja, Shelly Nachinuka, maarufu Biti Nachinuka alisema kina mama wanaongoza kwa malezi duni ya watoto.

“Ina maana gani mama kupewa madaraka katika familia lakini ndiye anayemlinda mtoto akitoroka usiku? Hata baba akisema anaambiwa - unamzuia nini au unamtaka?” alisema.

Alisema hata wanaowaambia watoto waandike sifuri kwenye mitihani ni kina mama.

Mkazi mwingine wa kata hiyo, Leticia Ng’ombo alisema wanawapiga wanaume pindi wanaporudi nyumbani wakiwa wamelewa na kuanza kutukana mbele ya watoto.

“Kama akirudi nyumbani na kuanza kuleta fujo mimi namkafua (nampiga) tu sana,” alisema.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Likunja, Joseba Mateka alisema mila hizo ndizo zinazochochea vipigo na hata kuvunjika kwa ndoa kila kukicha.

Wanakamati hao walisema miongoni mwa migogoro inayoongoza katika kata hiyo ni kuvunjika kwa ndoa na vipigo kwa wanaume.

Ofisa elimu wa kata hiyo, Mwajuma Ibadi alisema tatizo hilo limekuwa changamoto kubwa katika eneo hilo.

Meneja Ufuatiliaji na Tathmini wa Tamwa, John Ambrose alisema imebainika kuwa hivi sasa mila na desturi haziathiri wanawake pekee, bali hata wanaume.



Chanzo: mwananchi.co.tz