Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya watendaji Nemc yapigwa kalenda

29253 Pic+nemcTanzaniaWeb

Thu, 29 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es salaam. Upelelezi wa kesi ya kughushi saini ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba inayowakabili wafanyakazi sita wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc) bado haujakamilika.

Mbali na kughushi, washtakiwa hao pia wanakabiliwa na mashtaka mengine ikiwamo kula njama, kuwasilisha nyaraka za uongo, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kusababisha hasara ya Sh160milioni.

Leo Jumatano Novemba 28, 2018 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakili wa Serikali, Jenipher Masue, mbele ya hakimu mkazi mwandamizi, Augustina Mmbando amesema upelelezi wa kesi hiyo haujakamilia.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni ofisa mazingira Nemc, Deusdith Katwale (38) na  mtaalam wa Tehama, Luciana Lawi (33) wote wakazi wa Ubungo Msewe, ofisa mazingira, Magori Wambura (38) mkazi wa Bombambili.

Wengine ni katibu muhtasi, Edna Lutanjuka (51) mkazi wa Mbezi Beach St Gasper, msaidizi wa ofisi, Mwaruka Mwaruka (42) na ofisa mazingira, Lilian Laizer (27) wote  wakazi wa Ukonga Mombasa.

Wafanyakazi hao walifikishwa mahakamani hapo Oktoba 31, 2018 na kusomewa mashtaka sita ya uhujumu uchumi likiwamo la kughushi saini ya Makamba katika vyeti vya tathmini ya uharibifu wa mazingira.

Katika kesi hiyo washtakiwa watano wako nje kwa dhamana isipokuwa Wambura anayeendelea kusota rumande baada ya kukosa dhamana.

Hakimu Mmbando ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 12, 2018 itakapotajwa tena.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kati ya Septemba 27, 2016 na April Mosi, 2018 jijini Dar es Salaam walikula njama ya kutenda kosa la kughushi.

Katika shtaka la pili washtakiwa hao wanadaiwa kuwa  Oktoba 17, 2017 Dar es Salaam kwa udanganyifu walighushi cheti cha tathmini ya uharibifu wa Mazingira chenye namba ya usajili EC/EIA/3366 wakijaribu kuonyesha kuwa cheti hicho ni halali na kimetolewa na Nemc wakati wakijua si kweli.

Katika shtaka la tatu wanadaiwa kuwa Oktoba 2017 Dar es Salaam kwa nia ovu walighushi saini ya Makamba  katika cheti cha tathmini ya uharibifu wa mazingira chenye usajili namba EC/ EIA/3366 wakijaribu kuonyesha kuwa cheti hicho ni halali na kimetolewa na Nemc.

Katika shtaka la nne,  mshtakiwa Edna anadaiwa kuwa Oktoba 2017 katika ofisi za Nemc Dar es Salaam kwa kujua alitoa cheti cha kughushi cha tathmini ya uharibifu wa mazingira chenye namba ya usajili EC/EIA/3366 cha Oktoba 17,2017 kwa Deogratius Chacha, akijaribu kuonyesha kuwa cheti hicho ni halali na kwamba kimetolewa na Nemc.

Katika shtaka la tano, washtakiwa hao wote wanadaiwa kuwa kati ya Septemba 27 na Aprili 6, 2018 walijipatia kwa njia ya udanganyifu Sh160milioni kutoka kwa PMM Estate (2001) Ltd kwa madai kuwa wangeweza kufanya tathimini ya uharibifu wa mazingira na kumpatia cheti ambacho kinatolewa na Nemc.

Katika shtaka la sita washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Septemba27, 2016 na Aprili 6, 2018  Dar es Salaam waliisababishia Nemc hasara ya Sh160milioni.



Chanzo: mwananchi.co.tz