Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya wanaodaiwa kughushi nyaraka kujipatia Sh563 milioni yaunguruma

Hukumu Pc Data Kesi ya wanaodaiwa kughushi nyaraka kujipatia Sh563 milioni yaunguruma

Mon, 30 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imepanga Novemba 13, 2023 kuwasomea hoja za awali (PH) wafanyabiashara watatu na wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, wanaokabiliwa na mashtaka 16 yakiwemo ya kughushi nyaraka mbalimbali na kuisababishia hasara ya Sh563 milioni Benki ya NMB.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu, Oktoba 30, 2023 na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Fatma Waziri akishirikiana na Veronica Chimwanda, baada ya upelelezi wa shauri hilo kukamilika.

Washtakiwa hao ni Ernest Omalla, Juma Gululi na Zaid Bakari, ambao wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 186 ya mwaka 2023, iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili Waziri amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate kuwa, kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kuangalia kama wamekamilisha kuandaa nyaraka kwa ajili ya kuwasomea hoja za awali.

"Mheshiwa hakimu, bado hatujakamilisha kuandaa nyaraka kwa ajili ya kuja kuwasomea hoja za awali washtakiwa hao, hivyo tunaomba ahirisho fupi, ili tuje tuwasomee maelezo yao," amedai wakili Waziri.

Hakimu Kabate baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 13, 2023 itakapoitwa kwa ajili ya PH.

Pia hakimu Kabate alitoa masharti ya dhamana ambapo kila mshtakiwa anatakiwa kuwasilisha mahakamani hapo fedha taslimu Sh93 milioni au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.

Masharti mengi, washtakiwa hao wanatakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja wenye barua zinazotambulika kisheria, ambapo mmoja kati ya hao wadhamini anatakiwa kusiani dhamana ya maandishi ya Sh93 milioni.

Pia wadhamini hao wanatakiwa wawe ni kutoka ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Hata hivyo mshtakiwa Bakari amefanikiwa kupata dhamana huku wenzake wakishindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, kati ya mashtaka hayo 16 yanayowakabili washtakiwa hao; mashtaka sita ni ya kughushi nyaraka, mashtaka matano ni kuwasilisha nyaraka za uongo benki, mashtaka matatu ni kujipatia mkopo kwa njia ya udanganyifu na shtaka moja ni kuisababishia hasara Benki ya NMB.

Katika shtaka la kughushi nyaraka, Omalla, Gululi na Bakari wanadaiwa kati ya Februari Mosi na Februari 28, 2018 katika Jiji la Dar es Salaam kwa nia ya udanganyifu, washtakiwa walitengeneza nyaraka ya uongo ambayo ni leseni ya biashara yenye namba B 2791473 iliyotolewa Februari 21, 2018 ikionyesha imetolewa na Manispaa ya Ilala, wakati wakijua kuwa ni uongo.

Katika shtaka la kuwasilisha nyaraka za uongo kwenda benki, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Machi Mosi na Desemba 31, 2017, wanadaiwa kuwasilisha nyaraka ya uongo ambayo ni taarifa ya fedha na kuiwasilisha katika Benki ya NMB tawi la Kariakoo.

Katika shtaka la kujipatia mkopo kwa njia ya udanganyifu, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Machi Mosi na Agosti 30, 2018 katika jiji la Dar es Salaam, kwa lengo la kudanganya walijipatia Sh563, 351,689.67, kutoka Benki ya NMB, tawi la Kariakoo baada ya kuwasilisha taarifa ya uongo ya fedha, wakionyesha imetolewa Machi 3, 2018 na Benki ya NBC tawi la Victoria, wakati wakijua ni ongo.

Pia washtakiwa wanadaiwa kuisababishia hasara Benki ya NMB, ambapo katika tarehe hizo na kwa nia ovu, washtakiwa walijipatia Sh563, 351, 698 na hivyo kuisababishia benki ya NMB hasara.

Kwa mara ya kwanza, Omalla na Gululi walifikishwa mahakamani hapo Oktoba 18, 2023 na kusomewa na mashtaka yao, hata hivyo siku baadaye yaani Oktoba 23, mshtakiwa Bakari naye alifikishwa mahakamani na kuunganishwa na wenzake na kisha kusomewa mashtaka kama waliyosomewa wenzake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live