Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya wakurugenzi wa kampuni ya upatu yapigwa kalenda

29952 UPATU+PIC TanzaniaWeb

Mon, 3 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upelelezi wa  kesi ya utakatishaji fedha inayowakabili wakurugenzi wa Kampuni ya Rifaro Africa Limited, Jones Moshi (42) na James Gathonjia (35) bado haujakamilika.

Moshi na Gathonjia wanakabiliwa na mashtaka matatu, likiwamo la kuendesha biashara ya upatu pamoja na kutakatisha fedha kiasi cha Sh1.022 bilioni katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Desemba 3, 2018 na wakili wa Serikali,  Gloria Mwenda mbele ya hakimu mfawidhi,  Kelvin Mhina wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Gloria amedai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili kutajwa.

Hakimu Mhina baada ya kusikiliza maelezo hayo,  ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 17, 2018,  na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

Washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza  Kisutu  Novemba 19, 2018 kujibu mashtaka matatu katika kesi ya uhujumu uchumi namba  87/2018.

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa  kati ya Julai 14, 2014 na Julai 31, 2016 Jijini Dar es Salaam na maeneo mbalimbali Tanzania  walipanga njama ya kuendesha biashara ya upatu.

Shtaka la pili, wawili hao katika kipindi hicho na maeneo hayo, wanadaiwa kuendesha biashara ya upatu kwa kukusanya fedha kutoka kwa wananchi kwa ahadi kuwa fedha hizo zitazaa.

Washtakiwa hao katika shtaka la tatu ambalo ni utakatishaji wa fedha, wanadaiwa katika kipindi hicho na maeneo hayo, walijihusisha na miamala ya fedha ya moja kwa moja ya Sh1,022, 560, 854 kupitia akaunti namba 3301106013 iliyopo katika Benki ya Kenya Commercial (T)Ltd (KCB)  yenye jina la Rifaro Africa Limited wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya kuendesha biashara ya upatu.

Washtakiwa hao baada ya kusomewa mashtaka hayo hawakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu mahakama hiyo  haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz