Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya wakili anayedaiwa kughushi nyaraka yapamba moto

HUKUMU Kesi ya wakili anayedaiwa kughushi nyaraka yapamba moto

Mon, 10 Apr 2023 Chanzo: Mwananchi

Mtaalamu wa maandishi kutoka Jeshi la Polisi, Sajini kanzu Faustine Mashauri ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa, uchunguzi alioufanya kuhusu wakili wa kujitegemea, Benson Bwire (36) ulizingatia matakwa ya kisheria na kitaalamu.

Wakili Bwire, maarufu kwa jina la Kuboja anakabiliwa na mashtaka matatu, ikiwamo kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu Sh 4.6 milioni.

Katika kesi ya msingi inadaiwa Septemba Mosi, 2021 eneo la ofisi ya uwakili ya Kubojoka Wilaya ya Kinondoni, Bwire alighushi sahihi ya Dynes Mbaga huku akijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Inadaiwa tarehe kama hiyo maeneo hayo alijipatia Sh4.6 milioni kwa njia ya udanganyifu kwenye akaunti ya Benki ya CRDB yenye namba 015231759800 kutoka Lowgrich Case RTCS.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mosie Kaima mbele ya Hakimu Mwandamizi, Ramadhan Rugemalira mwishoni mwa wiki iliyopita, Sajini Mashauri ambaye ni shahidi alidai kuwa katika uchunguzi alioufanya alibaini tabia ya kisayansi iliyopo kwenye sahihi mbili, ya juu na chini zilikuwa zikifanana kitabia.

Alidai kuwa baada ya kukamilisha uchunguzi na kuandaa ripoti vielelezo alivirudisha ofisini kwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu (ZCO) kwa ajili ya hatua nyingine za kisheria.

Alidai katika shauri hilo jukumu lake kubwa lilikuwa ni kuchunguza saini na mihuri kwenye nyaraka alizokabidhiwa.

Baada ya kukamilisha kuhojiwa na upande wa Jamhuri, Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala alimhoji shahidi huyo maswali ya dodoso kuhusiana na ushahidi alioutoa.

Kibatala: Unasema ulipokea barua kutoka kwa ZCO kwa ajili ya kufanya uchunguzi?

Shahidi: Ndio nilipokea barua

Kibatala: Wewe ni mtunza barua za uchunguzi?

Shahidi: Mimi sio mtunza barua.

Kibatala: Ni sahihi kwenye maabara ya uchunguzi kuna kitabu cha kurekodi kila barua inayoingia na kutoka?

Shahidi: Ndio kipo.

Kibatala: Umekizungumzia hapa mahakamani?

Shahidi: Sijakizungumzia.

Kibatala: Kwa kuwa kitabu cha kutunza kumbukumbu ni kielelezo cha utunzaji barua umekitoa?

Shahidi: Sijakitoa kama kielelezo.

Kibatala: Hiyo barua inayoanzisha mchakato umeitoa kama kielelezo? Umetoa sababu ya kutoitoa kama kielelezo?

Shahidi: Sijatoa sababu.

Kibatala: Ni kweli au si kweli kwenye hiyo barua tungeona imeeleza uchunguzi ufanywe na mtu fulani?

Shahidi: Sio kweli barua inakuwa kwenye folda.

Kibatala: Tutaliona wapi tukitaka kuhakikisha?

Shahidi: Liko maabara Mahakama ikilihitaji nitalileta.

Wakili: Ulitoa maelezo kwa nini hukulileta tukaona nyaraka zinavyopelekwa hadi kufika?

Shahidi: Sikutoa.

Kibatala: Unafahamu hatua ya vielelezo hadi kufika kutolewa ushahidi?

Shahidi: Ndio.

Kibatala: Unafahamu umuhimu wake kwenye kesi?

Shahidi: Nafahamu kwa umuhimu wa maabara.

Kibatala: Ulinasema baada ya kukamilisha uchunguzi ulipeleka wapi?

Shahidi: Ofisi ya ZCO.

Chanzo: Mwananchi