Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili washtakiwa watatu akiwamo raia wa china kuendelea Januari 3

Mon, 24 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upande wa Mashtaka na ule wa utetezi katika kesi ya Uhujumu Uchumi inayowakabili washtakiwa watatu, akiwemo raia wa China, Yang Feng Glan (66), umepanga Januari 3, 2019 kuwasilisha majumuisho ya mwisho ya hoja za pande zote.

Mbali na Glan, maarufu kama Malkia wa Pembe za Ndovu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Salvius Matembo na Philemon Manase ambao wote wanatetewa na wakili Nehemia Nkoko.

Wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka ya kujihusisha na biashara haramu ya meno ya Tembo yenye thamani ya Sh13 bilioni kinyume cha sheria, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hatua hiyo, inatokana na upande wa mashtaka na ule wa utetezi kufunga ushahidi.

Mahakama hiyo iliwakuta washtakiwa wana kesi ya kujibu, baada ya upande wa mashtaka kupelekea mashahidi 11 ambao walitoa ushahidi  dhidi ya washtakiwa hao.

Wakili wa Serikali, Tuli Elea amedai mbele ya hakimu Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe kwa ajili kuwasilisha majumuisho ya mwisho ya hoja za pande  zote.

Hakimu Mmbando baada ya kusikiliza maelezo hayo aliahirisha kesi hiyo hadi, Januari 3,2019 ambapo pande zote zitawasilisha majumuisho ya kesi hiyo.

Miongoni mwa mashahidi waliotoa ushahidi katika kesi hiyo ni Fadhili Kayombo (31) ambaye aliwahi kuwa mhudumu wa vinywaji katika Mgahawa wa Beijing, unaomilikiwa na Glan, ulioko karibu na Moroco jiji hapa.

Kayombo ambaye ni shahidi wa nane katika kesi hiyo alidai alishtuka baada ya kuombwa abebe meno ya tembo kutoka katika gari ya mshtakiwa wa pili (Manase) na kuyapeleka katika chumba cha Glan kilichopo ndani ya Mgahawa wa Beijing.

Kayombo aliieleza mahakama kuwa alianza kazi katika mgahawa huo, mwaka 2010, kwa mshahara wa  Sh 60,000 kwa mwezi.

“Julai 2013, saa moja usiku, nikiwa naendelea na kuhudumia vinywaji  katika mgahawa huo ambao pia una ukumbi kwa ajili ya sherehe mbalimbali, ghafla alikuja  Philemon Manase (mshtakiwa wa pili) na kuniambia anaomba nimsaidie kushusha mzigo,”alidai Fadhili na kuongeza

 

“Ulikuwa katika gari yake aina ya Noah. Nilimuuliza ni mzigo gani? Akanijibu ni meno ya tembo, kiukweli nilishtuka, lakini Manase aliniambia hicho  iwe siri yangu na nisimwambie mtu, na kwamba nikimwambia tu mtu maisha yangu yatakuwa hatarini.” alidai

Baada ya kufika katika gari hiyo, Manase alifungua mlango wa gari na kuvuta mifuko miwili ya viroba(sandarusi) ambayo ilikuwa na vipande wa meno ya tembo.

“Tulibeba mfuko mmoja kwa kushikizana hadi katika chumba cha Glan kilichopo ghorofa ya kwanza katika mgahawa huo” alidai Fadhili.

Alieleza kuwa baada ya kufika chumbani kwa Glan, Manase alifungua mfuko huo na kutoa vipande vinne vya meno ya Tembo na kisha Glan alivikagua na baadae Manase alivirudishia katika mfuko wake na kuvifunga vizuri na kuviweka  pembezoni mwa kabati ya nguo.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao, wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22, 2014.

Wanadaiwa kuwa katika kipindi hicho walifanya biashara ya vipande 706 vya meno ya Tembo vyenye uzito wa kilogramu 1889 zenye thamani ya Sh 5.4 bilioni  bila ya kuwa na leseni iliyotolewa na Mkurugenzi wa Wanyama Pori.



Chanzo: mwananchi.co.tz