Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya uhujumu dhidi ya Sabaya na wenzake kusikilizwa mfululizo

SABAY ED.jpeg Kesi ya Sabaya uhujumu kusikilizwa mfululizo

Thu, 14 Oct 2021 Chanzo: ippmedia.com

KESI ya uhujumu uchumi namba 27 inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita, imepigwa kalenda hadi Oktoba 18, mwaka huu, itakaposikilizwa mfululizo kwa wiki nzima.

Ole Sabaya na wenzake, wanakabiliwa na mashtaka matano katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, likiwamo la matumizi mabaya ya madaraka, utakatishaji wa fedha, kujihusisha na vitendo vya rushwa, kuongoza genge la uhalifu na kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Mbali na Ole Sabaya, washtakiwa wengine katika shauri hilo ni Silvester Nyengu (26), Enock Togolani (41), Watson Mwahomange (27), John Odemba, Jackson Macha (29) na Nathan Msuya (31).

Akizungumza mahakamani huko jana, Hakimu wa Mahakama hiyo, Patricia Kisinga, alisema ameahirisha shauri hilo hadi Oktoba 18, mwaka huu na litasikilizwa mfululizo kwa wiki nzima.

“Kesi imeahirishwa kusikilizwa hadi Oktoba 18, mwaka huu, na kesi hii itasikilizwa kwa wiki nzima mfululizo,” alisema Hakimu Patricia.

Wakili wa Jamhuri, Neema Mbwambo, alidai shauri hilo lilikwenda kwa ajili ya kutajwa na aliiomba mahakama kupanga tarehe ya kusikilizwa kwa kesi.

Katika kesi hiyo, shtaka la kwanza ni la kuongoza genge la uhalifu kinyume cha sheria ya uhujumu uchumi kifungu cha 57(1) na 60(2) na linawakabili washtakiwa wote.

Ilidaiwa mahakamani huko kwamba Januari 22, mwaka huu, katika maeneo tofauti ya Jiji la Arusha, akiwa mtumishi wa serikali kwa nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Ole Sabaya na wenzake walifanya vitendo vya uhalifu kwa kujipatia fedha kiasi cha Sh. milioni 90 kwa manufaa yao.

Shtaka la pili ni la kujihusisha na vitendo vya rushwa na linamkabili mshtakiwa wa kwanza peke yake. Ilidaiwa mahakamani huko kwamba Januari 22 mwaka huu, eneo la kwa Murombo jijini Arusha, Ole Sabaya alijihusisha na vitendo vya rushwa kwa kumtaka Francis Mroso kumpatia fedha kiasi cha Sh. milioni 90 kwa kumshinikiza ili asitoe taarifa za jinai za mtu huyo za madai ya ukwepaji kodi.

Shtaka la tatu ni la kujihusisha na vitendo vya rushwa na linamkabili mshtakiwa wa kwanza peke yake. Inadaiwa kwamba Januari 22, mwaka huu, Ole Sabaya akiwa katika eneo la kwa Morombo jijini Arusha, alijihusisha na vitendo vya rushwa kwa kujipatia fedha kiasi cha Sh. milioni 90 kutoka kwa Francis Mroso, ili asitoe taarifa za jinai za mtu huyo za madai ya ukwepaji kodi.

Shtaka la nne ni la matumizi mabaya ya madaraka na linamkabili Ole Sabaya peke yake. Inadaiwa kuwa Januari 22 mwaka huu, Ole Sabaya, akiwa katika eneo la kwa Murombo jijini Arusha, alitumia vibaya nafasi yake ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, alimtisha Francis Mroso kumfungulia mashtaka ya kukwepa kodi.

Shtaka la tano ni la utakatishaji wa fedha na linawakabili washtakiwa wote saba. Inadaiwa Februari 22, mwaka huu, Ole Sabaya kwa kushirikiana na wenzake, wakiwa katika eneo la kwa Murombo jijini Arusha, walijipatia fedha kiasi cha Sh. milioni 90, wakitambua kwamba kufanya hivyo  ilikuwa ni zao la vitendo vya rushwa.

Chanzo: ippmedia.com